WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemtaka
Meneja wa TANESCO wilaya ya Ruangwa, Bw. Samuel Pyuza ahakikishe umeme
unapatikana mapema kwenye pampu ya maji ili kukamilisha mradi wa maji wa
Namahema ‘A’.
Ametoa wito huo jana jioni (Alhamisi,
Desemba 28, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa vijiji vya Namahema ‘A’ na
Namahema ‘B’ wilayani Ruangwa, mkoani Lindi waliofika kumsikiliza mara baada ya
kukagua mradi wa maji ambao umechukua miezi sita tangu uanze. Mradi huo
unatarajiwa kukamilika Januari 15, mwakani.
Mradi huo ambao hadi
kukamilika kwake utagharimu sh. milioni 244.52, unatarajiwa kuwahudumia wakazi 2,257
wa vijiji hivyo viwili ambao walikuwa wanasongamana kupata maji kutoka kwenye
kisima ambacho kilikuwa kinatumia pampu ya mkono. Kijiji cha Namahema ‘A’ kina
watu 1,668 na Namahema ‘B’ kina watu 589.
Waziri Mkuu ambaye yuko
kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka, ameanza ziara fupi ya siku tatu, kukagua
miradi ya maendeleo jimboni kwake katika wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi.
Jumla ya sh. milioni 189.93
zimeshatumika kwenye mradi huo ambazo ni sawa na asilimia 77.68 ya fedha ziliopangwa
kutumika. Fedha za mradi huo zimetolewa na Serikali Kuu kupitia Mfuko wa
Uwekezaji wa Maji wa Taifa (National Water Investment Fund).
Kazi ambazo zimekamilika
hadi sasa ni ujenzi wa vituo vya kuchotea maji (DP) 32; ujenzi wa mtandao wa
mabomba yenye urefu wa mita 6,460; tenki la kuhifadhia maji leye ujazo wa lita
50,000, ujenzi wa nyumba ya mitambo (pump house); ujenzi wa uzio (fence) kwenye
nyumba ya mitambo; ujenzi wa uzio (fence) kwenye tenki la kuhifadhia maji; na
ununuzi wa pampu na mota.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA,
DESEMBA 29, 2017.
No comments:
Post a Comment