HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 20, 2017

JESHI LA POLISI LAENDELEA NA UCHUNGUZI KUPOTEA KWA MWANDISHI WA HABARI

Jeshi la Polisi limesema linaendelea na uchunguzi wa kupotea mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Azory Gwanda na mwanachama wa Chadema, Ben Saanane.

Pia, limesema uchunguzi wa kushambuliwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na wa tuhuma za uchochezi zinazomkabili Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa unaendelea.

Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Boaz amesema hayo leo Jumatano Desemba 20,2017 alipozungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

"Uchunguzi wa hili la mwandishi mwenzenu unaendelea ziko taratibu ambazo sisi polisi tunapaswa kuzifuata, hivyo muwe na subira wakati tukiendelea," amesema DCI Boaz.

Hadi leo, Gwanda amefikisha siku 30 tangu alipotoweka baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana akiwa Kibiti mkoani Pwani.

Kuhusu Saanane aliyepotea tangu Novemba,2016 Boaz amesema uchunguzi unaendelea.

Ameomba ushirikiano kutoka kwa wananchi akitaka wenye taarifa kuziwasilisha kwao.

DCI Boaz akizungumzia tukio la kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi Lissu Septemba 7,2017 amesema suala hilo limezungumzwa sana na viongozi wengine na kuomba waachwe ili uchunguzi uendelee.

Kuhusu tuhuma za uchochezi anazokabiliwa nazo Lowassa, DCI Boaz amesema kuna taarifa wanaendelea kuzikusanya kwa kuwa kulikuwa na upungufu, hivyo wakikamilisha watachukua hatua zaidi. MWANANCHI

No comments:

Post a Comment

Pages