HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

October 13, 2025

Mbeto : Zanzibar ni nchi Huru

Na Mwandishi Wetu , Zanzibar

Chama Cha Mapinduzi  kimekitaka ACT  Wazalendo kutoidanganya dunia na kutoa madai  kuwa Zanzibar inadai  haki zake hivyo yeye na wenzake  wako katika juhudi za  kuinusuru Zanzibar.

CCM kimesisitiza  Zanzibar ina  uhuru kamili , kila Mzanzibari anapata Haki za  kujitawala  tokea Januari 12 Mwaka 1964.

Katibu wa Kamati Maalum  ya NEC  Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Khamis Mbeto  Khamis, ameeleza hayo huku akikitaka   ACT Wazalendo  kuacha  kuipotosha jamii na ulimwengu.

Mbeto alisema baada ya Miaka 104  Zanzibar  ikitawaliwa chini ya  Ufalme  kwa kushirikiana na  Uingireza,  chama cha Ukombozi  cha Zanzibar ASP,  kimefanikiwa kutwaa Madaraka  ya Dola na kuanza kujitawala.

Alisema chini   ASP na sasa utawala ukiongozwa na  CCM, Zanzibar itabaki kuwa  huru yenye Serikali yake, Mahakama, Bendera, Rais wake, Katiba, Watu na Baraza la Wawakilishi Zanzibar. 

"Zanzibar  haihitaji mbeleko ya  Ukombozi mwingine ili ijitawale. Kupitia Mapinduzi  Matukufu ya Wazanzibari wameshagomboka, wako Huru wakijiitawala bila kuingiliwa na yeyote Duniani" alisema Mbeto.

Katibu  Mwenezi huyo alisema  matokeo ya  kuwepo kwa kabrasha la  makubaliano ya Muungano kati ya Mataifa huru ya Tanganyika na Zanzibar hatimae nchi hizo ziliungana kwa hiyari katika utaratibu wa kawaida unaofahamika   duniani. 

"Haukuwa  uamuzi wa  uchuro au wenye  na majuto   Zanzibar kuungana na Tanganyika  kupata Taifa moja. Imepata Bendera moja  na kiti  kimoja  Umoja wa Mataifa  (UN)"alisema Mbeto.

Akieleza kwa undani, alisema hata ingetokea Mwaka 1963 kwa Serikali ya ZNP  na ZPPP ingeamua kuungana na nchi yoyote Afrika, maamuzi hayo  yangeheshimika pia  kutambuliwa na Umoja  wa Mataifa.

Vile vile,  Mbeto  alisema Zanzibar baada ya Mwaka 1964 si  Koloni   la Nchi  yoyote Duniani, ni nchi  Huru inayojiamulia mambo yake yenyewe.

"Dunia  inaishuhudia Zanzibar kuitambua iko huru. Midhali CCM kitaendelea kuaminiwa na wananchi kupitia  uchaguzi wa kidemokrasia kitatekeleza matakwa ya kuwa na Taifa  moja  Tanzania" alieleza .

Katibu huyo Mwenezi, alimtaka mgombea Urais kwa kofia ya ACT, Othman Masoud  Othman, aendelee kunadi Sera za ACT kama zipo  ili kipate ridhaa bila kutumia  mbinu za kusema  uongo majukwaani.



No comments:

Post a Comment

Pages