WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imebaini kwamba
maeneo ya bahari kuu, bandari, vituo vya mabasi na viwanja vya ndege
yanayotumika sana katika kupitisha dawa za kulevya.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema wafanyabiashara, wasambazaji na
watumiaji wa dawa za kulevya wameendelea kukamatwa, lengo ni kuhakikisha
biashara hiyo inamalizika nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 13,
2018) wakati akikabidhi gari kwa Kamishna Generali wa Mamlaka ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya Bw. Rogers Siyanga
kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Amesema mbali na kukamata meli, pia Serikali imewakamata wasambazaji
pamoja na kundi kubwa la wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara ya dawa za
kulevya sambamba na watumiaji, lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa salama na
kizazi chenye uwezo wa kuzalisha mali.
Waziri Mkuu amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika vita
dhidi ya dawa za kulenya, ambapo hivi karibuni imekamata meli nyingi, moja
ilikiwa inatokea pwani ya Msumbiji na ilikamatiwa maeneo ya Mtwara ikiwa na
dawa nyingi za kulevya.
“Niwakati wa Serikali kuendelea kuiwezesha Mamlaka ya
Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya na leo hii tunawakabidhi gari hili
jipya kabisa ili iweze kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake ipasavyo.”
Pia Waziri Mkuu amewataka Watanzania waachane na biashara ya
dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na kazi
ya kusambaza, kuzalisha na kutumia na watakaokamatwa wakijihusisha nayo
watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Amesema kwa sasa Serikali inajenga maabara ambayo itatumiwa
na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa ajili ya kufanya
uchunguzi wa dawa wanazozikamata.
Waziri Mkuu amesema wananchi wanatakiwa kushirikiana na
Serikali katika vita dhidi ya dawa za kulevya kwa kutoa taarifa mara wanapowabaini
wafanyabiashara, watumiaji na wasambazaji wa dawa hizo. Pia wahakikishe
wanawalinda vijana ili wasijihusishe na dawa za kulevya.
Kwa upande wake Siyanga aliishukuru Serikali kwa kuipatia
mamlaka hiyo gari, ambapo alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi waachane na
biashara ya dawa za kulevya. Alisema wanapambana kuhakikisha dawa za kulevya
ili zisiingie nchini.
Alisema mbali na kudhibiti biashara hiyo, pia wanatoa elimu juu
ya madhara ya matumizi ya dawa za kulevya vikiwemo vitendo viovu vinavyofanywa
na watumiaji ili wachukie na waache kutumia dawa hizo.
Pia wanafanya kazi ya kuwahudumia watu walioathirika na
matumizi ya dawa za kulevya, hivyo aliwaomba wananchi kutowanyanyapaa waathirika
na badala yake wawapeleke katika vituo maalumu vya kutolea huduma za methadone.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 13,
2018.
No comments:
Post a Comment