WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
Mawaziri wa Afya kutoka nchi tisa za Afrika kutoa mapendekezo ya namna ya
kutokomeza magonjwa yasiyo ambukiza kwa wakuu wa nchi hizo ili yafanyiwe kazi.
Aliyasema hayo jana jioni (Jumatatu,
Machi 19, 2018) wakati akifungua Mkutano wa 65 wa Mawaziri wa Afya kutoka nchi
tisa wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika Mashariki, Kati na Kusini (ECSA-HC)
Alisema magonjwa yasiyo ambukiza ni
miongoni mwa magonjwa ambayo yameendelea
kuwatesa wananchi kwa kiasi kikubwa katika nchi nyingi za Bara la
Afrika, hivyo vema mawaziri hao wakatoa mapendekezo ya namna ya kuyatokomeza.
Waziri
Mkuu alisema magonjwa hayo yanaweza kudhibitiwa kwa kuhamasisha wananchi
kuboresha lishe na kusisitiza ulaji wa vyakula bora, kufanya mazoezi na
kubadili mitindo ya maisha.
“Magonjwa
yasiyoambukiza yanaongoza kwa kusababisha vifo katika baadhi ya nchi wanachama
wa ECSA. Magonjwa haya yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na mabadiliko ya mfumo
wetu wa lishe na maisha, hivyo ni muhimu suala hili likatafutiwa ufumbuzi.”
Waziri Mkuu alisema
magonjwa yasiyoambukiza pamoja na magonjwa mengine ya milipuko kama ebola, homa
ya bonde la ufa, dengue, homa ya manjano yamekuwa kikwazo cha maendeleo kwa
katika baadhi ya nchi.
Pia, Waziri Mkuu
aliongeza kuwa sekta ya afya ni muhimu kwa ajili ya kuboresha maendeleo ya nchi
zote zikiwemo zilizoendelea na zinazoendelea, hivyo changamoto zote
zinazoikabili zinapaswa zipewe kipaumbele katika utatuzi.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Jinsia, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto, Bibi Ummy
Mwalimu alisema malengo ya mkutano huo ni kuzungumzia changamoto mbalimbali
zinazohusu sekta ya Afya na kuyapatia ufumbuzi.
Mkutano huo ulihudhuriwa
na Mawaziri wa Afya kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afya kwa nchi za Afrika
Mashariki, Kati na Kusini ambazo ni Tanzania,
Malawi, Lethoto, Uganda, Kenya, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Muwakilishi kutoka
nchini Mauritious.
Pia Katibu wa jumuiya
hiyo Profesa Yoswa Dambisya, Muwakilishi wa Benki ya Dunia Dkt. Paolo Belli pamoja
na wadau wa sekta ya afya kutoka nchi hizo.
IMETOLEWA NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE,
MACHI 20, 2018.
No comments:
Post a Comment