WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kuimarisha vyama vya msingi vya
ushirika vya mazao ya kilimo na masoko vinavyozalisha mazao ya kimkakati ya
biashara ya pamba, kahawa, korosho, chai na tumbaku.
Amesema katika
mwaka 2018/2019, Serikali inalenga kuimarisha masoko ya mazao hayo kwa
kuhamasisha mfumo wa stakabadhi ghalani ambapo mazao hayo yatazalishwa na
kuuzwa kupitia vyama vya ushirika kwa njia ya minada.
Ametoa kauli
hiyo leo (Jumatano, Aprili 4, 2018) Bungeni mjini Dodoma, wakati akiwasilisha
taarifa ya mapitio ya utekelezaji wa kazi za Serikali kwa mwaka 2017/2018 na
mwelekeo wa kazi za Serikali kwa mwaka 2018/2019 kwenye mkutano wa 11 wa Bunge.
Waziri Mkuu
amesema pamoja na hatua hizo, Soko la Bidhaa ambalo limeshaanzishwa, litasaidia
sana kuimarisha masoko ya mazao kwani yatakuwa yanauzwa kwa njia ya ushindani
mkubwa huku wakulima wanaozalisha kwa ubora wakinufaika na bei ya juu zaidi.
“Serikali imeamua kuweka mkazo maalum wa
kuyaendeleza kwa kasi mazao matano ya biashara ambayo ni chai, kahawa, korosho,
pamba na tumbaku. Lengo ni kuongeza mapato ya wakulima, kuwa chanzo cha
kuaminika cha malighafi katika uchumi wa viwanda, na kuendelea kuwa chanzo
kikuu cha ajira na fedha za kigeni.
Amesema uamuzi wa kuongeza usimamizi katika
uzalishaji wa mazao hayo makuu ya biashara unatokana na ukweli kwamba, kwa
kipindi kirefu uzalishaji ulishuka kutokana na changamoto kadhaa.
“Miongoni mwa changamoto hizo ni kupungua tija
katika uzalishaji, baadhi ya wakulima kuacha kulima mazao hayo kutokana na
kukata tamaa kwa sababu mbalimbali zikiwemo vyama vya ushirika kutotekeleza
vema wajibu wao, wizi, dhuluma na pia ushiriki mdogo wa maafisa kilimo katika
kusimamia kilimo cha kitaalamu,” alisema.
Alizitaja sababu nyingine za kushuka uzalishaji wa
mazao hayo kuwa ni huduma zisizoridhisha za ugani na utafiti, ukosefu wa
pembejeo bora, utitiri wa tozo na wingi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya
ushirika.
Akitolea mfano, Waziri Mkuu alisema uzalishaji wa
pamba ulipungua kutoka tani 456,814 mwaka 2013/2014, hadi tani 282,809 mwaka
2015/2016. Kwa upande wa tumbaku, Waziri Mkuu alisema uzalishaji katika kipindi
cha miaka minne ulishuka kutoka tani 126,624 mwaka 2010/2011 hadi kufikia tani
60,929 mwaka 2015/2016.
“Serikali imechukua hatua za kuimarisha utawala bora
kwenye vyama vya ushirika kwa kusimamia chaguzi za vyama 2,537, chaguzi za
viongozi wa bodi za vyama vya ushirika 532 na kufanya kaguzi katika vyama vya
ushirika 2,896 vikiwemo vyama vikuu. Kazi za kusimamia vyama vya ushirika
zinaendelea,” alisema.
Wakati
huohuo, Waziri Mkuu alisema Serikali
inasimamia uendelezaji wa mazao hayo moja kwa moja kupitia maafisa kilimo na
Bodi za Mazao na kwamba imechukua hatua za kufuta baadhi ya tozo zilizokuwa
kero katika mazao makuu ya biashara pamoja na kuhakikisha kwamba mauzo
yanafanyika kwa njia ya wazi na inayoleta ushindani.
“Kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali
kusimamia mazao makuu ya biashara, tayari tumeanza kuona matokeo chanya kwa
kuongezeka uzalishaji wake. Kwa mfano, hadi mwezi Machi 2018, uzalishaji wa
mazao ya asili ya biashara ulifikia tani 804,025. Uzalishaji huu unaashiria
ongezeko la mavuno ikilinganishwa na mwaka 2016/2017. Ongezeko hilo la
uzalishaji wa mazao ya biashara linakwenda sambamba na kuimarika kwa mwenendo
wa bei za mazao hayo hususan korosho na kahawa,” alisema.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
S.
L. P. 980,
41193 - DODOMA.
JUMATANO,
APRILI 4, 2018
No comments:
Post a Comment