HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 20, 2018

WAZIRI KIGWANGALA MGENI RASMI Ngorongoro Race 2018

NA MWANDISHI WETU, KARATU

MASHINDANO ya Ngorongoro Race 2018 yanatarajiwa kurindima mjini hapa leo huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamis Kigwangala.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana, Mkurugenzi wa Ngorongoro Race, Meta Petro, Waziri Kigwangala ndiye atayeanzisha mbio za Kilomita 21 zitakazoanzia kwenye lango la kuingilia na kutokea Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.

Meta, alisema mbio hizo zinabeba kauli mbiu isemayo; `Kimbiza Jangili’ ikiwa na lengo la kuhamasisha vita dhidi ya vitendo vya ujangili dhidi ya rasilimali za Taifa, hususan wanyamapori.

Alisema Kigwangala amethibitisha kuanzisha mbio hizo na kukabidhi zawadi kwa washindi pale zitakapokamilika na washindi kujulikana.

Mkurugenzi huyo, alisema mbio hizo zitaanzia katika lango kuu la kuingilia na kutokea katika Bonde la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), ambao ndio pia ni wadhamini wakuu wake na kumalizikia katika viwanja vya Mazingira Bora katikati ya Mji wa Karatu.

Alisema kuwa wanatarajia mbio za mwaka huu zitakuwa na ushindani wa hali ya juu, hasa ukizingatia zitashirikisha wanariadha wengi zaid ya 500 walioshiriki mwaka jana.
Nyota mbalimbali wa mbio nchini wanatarajia kushiriki mbio hizo wakiwemo washindi wa mwaka jana kwa upande wa kiume na kike, Faraja Lazaro wa JKT na Failuna Abdi wa Talent Club ya Arusha, ambao walishinda mbio hizo kwa kutumia saa 1:03.42 na 1:03.52.

Mshindi wa kwanza wa mbio hizo kwa upande wanaume na wanawake, kila mmoja ataondoka na Sh milioni 1 wakati mshindi wa pili atabeba Sh 500,00 huku watatu Sh 250,000, mshindi wan ne atapewa 100,000 na watano Sh 80,000.

Kwa mujibu wa waandaaji, mbio za mwaka huu zitakuwa na zawadi hadi kwa mshindi wa 15 huku mshiriki yeyote atakayemaliza mbio hizo katika nafasi yoyote, atapewa medali pamoja na fulana kama kumbukumbu za kushiriki mbio hizo.

Mbali na kilometa 21 pia kutakuwa na mbio za kilometa tano, ambapo kwa mara ya kwanza washindi watapewa zawadi, kwani mbio hizo ni za kujifurahisha na waandaaji wamekuwa hawatoi zawadi kwa washindi.

Mshindi wa kwanza wa kilometa tano ataondoka na kitita cha Sh 200,000 wakati mshindi wa pili ataondoka na Sh 100,000 huku mshindi watatu kwa kila upande, atasepa na Sh 50,000.

Pia, kutakuwa na mbio za watoto wadogo, ambao watachuana katika umbali wa kilometa 2.5, ambapo mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 50,000, huku wa pili atabeba Sh 40,000 na watatu Sh 30,000.

Mbali na NCAA, wadhamini wengine ni Kampuni ya Vinywaji Baridi ya Bonite Botlers.

No comments:

Post a Comment

Pages