WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema kuvumiliana na kustahamiliana ndiko
kunakolifanya Taifa la Tanzania kuwa mfano wa kuigwa na kimbilio la wale
waliovurugikiwa na amani katika nchi zao.
Kadhalika,
uwepo wa amani nchini si tu unatoa fursa ya kutekeleza majukumu ya
kiuchumi na kijamii bila hofu bali pia ni sababu muhimu ya wenzetu
wengine kutoka nje kuona fursa ya kuwekeza na kushirikiana nasi katika
kujenga maendeleo ya nchini.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Juni 28, 2018) wakati akizindua
Umoja wa Kimataifa wa Wabunge Wapenda Amani tawi la Tanzania (IAPP),
kwenye mkutano uliyofanyika katika ukumbi wa Msekwa Bungeni, jijini
Dodoma.
Amesema
amani na utulivu ni tunu kubwa sana katika jamii yoyote ile Duniani na
Tanzania muda wote imeendelea kuenzi tunu hiyo iliyojengwa kwenye
misingi imara kupitia waasisi wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na
Sheikh Abeid Amani Karume.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Shirikisho la Amani kwa
Wote (Universal Peace Federation (UPF), ambalo lilianzishwa kwa lengo
la kumkomboa binadamu kutoka katika udhalili wa kukosa mahitaji muhimu.
“Hili
linadhihirika kupitia mipango ya shirikisho hilo ya kushirikiana na
jamii nyingine katika kuimarisha sekta zenye kugusa maisha ya watu wengi
kama vile kilimo, mazingira, afya, elimu, miundombinu na nyinginezo,”
amesema.
Hata
hivyo, Waziri Mkuu amesema utekelezaji wa mipango hiyo utategemea kwa
kiasi kikubwa uwepo wa amani na utulivu katika jamii husika, ambapo
amewahakikishia kwamba Serikali ipo tayari na itaendelea kushirikiana
nao katika nyanja hizo za kijamii na maeneo mengine kwa ajili ya kulinda
maslahi ya pande zote mbili na kuwaletea maendeleo wananchi.
“Nitoe
rai kwa Waheshimiwa Mawaziri wa sekta husika kwamba hakikisheni
mnaanzisha mazungumzo na wawakilishi wa UFP nchini kwa lengo la kuona
namna nzuri ya kuchangamkia fursa zinazopatikana kupitia shirikisho hilo
hususan katika sekta za kilimo, elimu, afya, mazingira na miundombinu,”
amesema.
Awali,
Mwenyekiti Mwanzilishi wa IAPP, Bw. Mussa Ntimizi amesema Shirikisho la
Amani kwa Wote litasaidia nchi kuboresha miradi mbalimbali ya
maendeleo kama ya kilimo, afya kwa sababu hakuwezi kuwa na amani bila
maendeleo.
Naye,
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Bw. William Ngeleja amesema Shirikisho
la Amani kwa wote limetenga dola bilioni tatu kwa ajili ya kusaidia
sekta ya afya katika nchi 10 za Bara la Afrika na Tanzania ikiwemo.
Katika hafla hiyo Waziri Mkuu amepewa tuzo ya Balozi wa Amani na Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh. Viongozi wengine walipewa tuzo hiyo ni pamoja na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu
Spika Dkt. Tulia Ackson, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo,Bw. William
Ngeleja Katibu Msaidizi wa umoja huo Bibi Anna Lupembe, Mweka hazina
Bibi Ritta Kabati.
Baada
ya kukabidhi tuzo hizo, Dkt. Walsh shirikisho lao linahitaji kufanya
kazi nna Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia kwa ajili ya kuboresha
maendeleo na amani. Amesema katika Taifa kukiwa na maendeleo amani
lazima itakuwepo.
Hafla
hiyo imehudhuriwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai, Naibu Spika Dkt. Tulia
Ackson, Mwenyekiti wa Shirikisho la Amani kwa Wote (UPF), Dkt. Thomas Walsh, Katibu
wa Shirikisho la Amani kwa Wote Kanda ya Afrika (UPF_Afrika), Bw. Adama
Doumbia, Katibu wa Shirikisho la Amani kwa Wote Tanzania
(UPF_Tanzania), Bw Stylos Simbamwene,
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 - DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 28, 2018.
No comments:
Post a Comment