MOSCOW, RUSSIA
WAKATI mabingwa watetezi wa Kombe la Dunia wakiaga
mashindano hayo jana kwa kipigo cha mabao 2-o kutoka kwa Korea Kusini,
wawakilishi pekee wa Afrika walio na matumaini ya kusonga mbele, Senegal,
wanashuka dimbani Juni 28, 2018 kuivaa Colombia.
Mashujaa wa Korea Kusini, ambao walikuwa
wanakamilisha ratiba tu jana, walikuwa ni Kim-Young Gwon na Son-Heung Min,
ambao walifunga mabao mawili yaliyofanya Ujerumani kufuata nyayo za Ufaransa,
Italia na Hispania, watetezi walioshia hatua ya makundi.
Ufaransa ambao walikuwa ni mabingwa wa fainali za 1998, waliishia hatua ya
makundi mwaka 2002, kama ilivyokuwa kwa mabingwa wa mwaka 2006, Italia
walioshia hatua ya makundi katika fainali za 2010. Nao Hispania waliotwaa taji 2010,
walichemka katika utetezi mwaka 2014.
Tukirudi katika pambano la Senegal, maarufu kama
Simba wa Teranga, ndio nchi pekee ya Afrika inayoweza kufuzu hatua ijayo ya
fainali hizo, baada ya wawakilishi wengine Misri, Morocco, Nigeria na Tunisia
kuyaaga mashindano hayo baada ya kuvurunda katika mechi zao kweye makundi.
Simba wa Teranga, wanaonolewa na nyota wa zamani
timu hiyo, Alliou Cisse, wanashuka dimbani Cosmos Arena mjini Samara, kuwavaa
Colombia katika mtifuano wa Kundi H, ambako inasaka sare tu dhidi ya miamba
hiyo ili kufikisha alama tano na kufuzu 16 Bora.
Wakali hao wanashuka dimbani kuivaa Colombia wakiwa
na pointi nne, ilizopata kwa ushindi wao wa mabao 2-1 dhidi ya Poland na sare
ya 2-2 walipoumana na Japan, ambako leo wanapambania sare ili kutinga hatua
ijayo ya fainali hizo.
Colombia wana pointi tatu walizopata katika ushindi
wa mabao 3-0 dhidi ya Poland, hivyo watakuwa wakipambana kuichapa Senegal, ili
kutinga mtoano wa 16 Bora ya fainali hizo za 21 zinazoendelea katika viwanja
mbalimbali nchini Russia.
Wawakilishi wengine wa Afrika, Tunisia, wanamaliza
mechi zao za Kundi G leo kwa kushuka dimbani kuumana na Panama, pambano la
kukamilisha ratiba baada ya kuziaga fainali hizo na kuzifuata Misri
(iliyomaliza mkiani Kundi A), Morocco (mkiani Kundi B), Nigeria (nafasi ya tatu
Kundi D) na Tunisia (mkiani Kundi H).
Mwamuzi wa mechi ya Ujerumani na Korea Kusini, Mark Geiger, akiwataka wachezaji wa Korea Kusini waliokuwa wanashangilia kurudi uwanjani.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani, Mesut Ozil, akiwa ameduwaa baada ya kuchapwa na Korea Kusini mabao 2-0.
Mshambuliaji wa tim u ya taifa ya Korea Kusini, Kim Young-gwon, akishangilia baada ya kuifungia timu yake bao la kwanza dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Dunia la Fifa.
Sami Khedira, akiwa amejifunika uso baada ya kupata kichapo kutoka kwa timu ya Korea Kusini. Mwamuzi wa mechi ya Ujerumani na Korea Kusini, Mark Geiger, akiwataka wachezaji wa Korea Kusini waliokuwa wanashangilia kurudi uwanjani.
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Korea ya Kusini, Son Heung, akiwaangalia mashabiki huku akibubujikwa na machozi ya furaha baada ya kuifungia timu yake bao la pili dhidi ya Ujerumani katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Dunia.
No comments:
Post a Comment