Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (kushoto), akizungumzia miradi ya
miundombinu ikiwemo ya Reli ya Kisasa kwa kiwango cha kimataifa, katika
kuchochea maendeleo ya kiuchumi, wakati wa Mkutano na Makamu wa Rais wa
Afreximbank Bw. Amr Kamel, uliofanyika Bali Indonesia, kulia ni Kamishna wa
Fedha za Nje wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. John Rubuga.
Meneja wa Afreximbank Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Kudakwashe Matereke, akieleza jambo wakati wa Mkutano kati ya Makamu wa Rais wa Afreximbank Bw. Amr Kamel na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hawapo pichani), mjini Bali Indonesia wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa–IMF.
Meneja wa Afreximbank Kanda ya Afrika Mashariki Bw. Kudakwashe Matereke, akieleza jambo wakati wa Mkutano kati ya Makamu wa Rais wa Afreximbank Bw. Amr Kamel na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (hawapo pichani), mjini Bali Indonesia wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa–IMF.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango (kushoto), na Makamu wa Rais wa Afreximbank, Amr Kamel, wakipeana mkono baada ya kumalizika kwa mkutano kati yao uliofanyika mjini Bali Indonesia wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). (Picha na Wizara ya Fedha na Mipango).
Na WFM, Mjini Bali Indonesia
African Export Import Bank
(Afreximbank) ya Misri, imeonyesha nia ya kuipatia Tanzania mkopo wa zaidi ya Shilingi
trilioni moja (dola za Marekani zaidi ya milioni 500) kwa ajili ya kutekeleza
miradi ya kipaumbele hasa ya miundombinu ya reli na kujenga vituo vya biashara
(SEZ and Industrial parks).
Hayo
yalibainishwa mjini
Bali Indonesia, na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Isdor Mpango
baada
ya Mkutano na Makamu wa Rais wa Afreximbank Bw. Amr Kamel, uliofanyika
wakati wa mikutano ya mwaka ya Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha
la
Kimataifa (IMF) ikiendelea.
Waziri
Mpango, alisema
kuwa Afreximbank imethibitisha kuwa ipo tayari kutoa mkopo wa dola za
Marekani milioni 125 (takribani Shilingi bilioni 285.9) kwa ajili
ya ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Kimataifa (SGR), kipande cha
Morogoro hadi Makutupora mkoani
Dodoma.
“Afreximbank wanania pia ya
kutoa dola milioni 400 (takribani Sh.
Bilioni 914.9) ambazo wanaweza kutukopesha kwa ajili ya kugharamia miradi ya
miundombinu itakayorahisisha biashara kati ya Tanzania na nchi jirani na Bara
la Afrika kwa ujumla, ili kuchochea kasi
ya ukuaji wa biashara katika nchi hizo kwa lengo la kuondoa umasikini”, aliongeza
Dkt. Mpango.
Alisema kuwa kwa kuwa
tayari Tanzania ilikuwa na mkakati wa kufungua vituo vya biashara katika mikoa ya
Dar es Salaam, Mtwara na mikoa mingine, suala la mkopo huo ni fursa kubwa
kwa maendeleo ya nchi, hivyo jambo hilo
litafanyiwa kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji na Sekta Binafsi, ili Taifa liweze kunufaika
na fedha ambazo benki hiyo ipo tayari kuzitoa.
Aidha, amesema kuwa katika majadiliano na benki hiyo kuna umuhimu
wa kuangalia namna ya rasilimali fedha ambazo Benki Kuu za nchi mbalimbali za
Afrika zimekuwa zikiwekeza nje ya Bara hilo, ili ziweze kuwekezwa kwenye benki
za Afrika kama Afreximbank ili kuleta maendeleo kwa haraka katika Bara hilo.
Vile vile benki hiyo
imeikaribisha Tanzania kushiriki mkutano wa biashara utakaofanyika mwezi
Desemba mwaka huu mjini Cairo Misri, ambapo kwa upande wa Tanzania ni fursa kwa
Makampuni ya umma na binafsi kutangaza bidhaa mbalimbali zinazozalishwa kwa
lengo la kukuza biashara ndani ya Bara la Afrika.
Makamu wa Rais wa
Afreximbank Bw. Amr Kamel, alisema kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi za
kimkakati kwa kuwa ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi jirani, hivyo
Afreximbank imeamua kusaidia miradi mbalimbali ya ujenzi wa miundombinu ili
kuharakisha maendeleo ya nchi ya Tanzania na nyingine.
Waziri Dkt. Mpango
ameishukuru Benki hiyo kwa kuisaidia Tanzania katika mkakati wa kufikia uchumi
wa kati unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025, hivyo kuwa Taasisi yenye tija si
tu kwa maendeleo ya Tanzania lakini pia kwa Bara la Afrika.
Imetolewa
na :-
Kitengo
cha Mawasiliano Serikalini
Wizara
ya Fedha na Mipango
Bali,
Indonesia
No comments:
Post a Comment