Katibu, Ofisi ya Rais, Tume
ya Utumishi wa Walimu, Winifrida Rutaindurwa amewashauri watendaji wanaojikita
katika kutoa vitisho kwa walimu badala ya kutafuta mbinu bora za kuwasaidia
kuacha kufanya hivyo ili Walimu wasijiingize katika makosa ya kinidhamu kwa
kisingizio cha kuogopa vitisho.
Rutaindurwa ametoa kauli
hiyo hivi karibuni jijini Dodoma alipokutana na Maafisa Elimu, Wathibiti Ubora,
Waratibu Elimu Kata (Maafisa Elimu Kata), Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kutoka
Halmashauri ya Jiji la Dodoma.
Lengo la mkutano huo
lilikuwa kuwaelimisha Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule kuzingatia maadili na nidhamu kwa mujibu wa Sheria, Kanuni, Taratibu pamoja na Miongozo
mbalimbali inayotolewa na Serikali.
Alisema kuwa walimu
hawapaswi kuishi kwa hofu kila wakati kutokana na vitisho wanavyopata kutoa kwa
baadhi ya watendaji badala yake wanatakiwa kutekeleza majukumu yote kwa
kuzingatia misingi na taratibu za utumishi wao.
Rutaindurwa alionesha
kukerwa na baadhi ya watendaji wanaowasimamia walimu ambao kazi yao ni kutoa vitisho
vya kuwafukuza kazi au kuwavua madakara endapo malengo flani hayatafikiwa bila
kusaidia kutatua changamoto zinazokabili Walimu kufikia malengo.
“Unakuta mtu anakuambia
wanafunzi wote wasipofaulu nakushusha cheo au nakufukuza lakini wala hamsaidii
mkuu wa shule au mwalimu mkuu kutatua baadhi ya changamoto ambazo zipo ndani ya
uwezo wake” alisema.
Aliongeza kuwa vitisho
hivyo vimesababisha baadhi ya walimu kujikuta wakitenda makosa ya kinidhamu ili
waonekane wamekidhi matakwa ya wanaowasimamia na matokeo yake wanachukuliwa
hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi.
“Sasa walimu lazima
mtumie akili na sio kufanya vitu ili umridhishe mtu wakati unajiingiza katika
hatari. Ukienda kuiba mtihani na kuwapa majibu wanafunzi ili ionekane shule
yako imefanya vizuri hautabaki salama” alisema.
Aliongeza kuwa,
“napenda muelewe kuwa ukitenda kosa usifikirie utakuja kujitetea kwa kusema
nilifanya kwa vile niliambiwa nikaogopa, sisi tunakushughulikia wewe uliyekiuka
maadili na taratibu za ualimu, unawajibika mwenyewe.”
Amesisitiza kuwa ni
lazima mwalimu atekeleze wajibu wake kikamifu katika kufundisha ili wanafunzi
wafaulu lakini baadhi ya watendaji nao hawapaswi kutoa vitisho vinavyomfanya
mwalimu ashawishike kutenda makosa ili tu afikie malengo.
“Nimefurahi kwa kuwa
Maafisa Elimu na Wathibiti Ubora mpo hapa. Nipende kuwasihi msiwatishe walimu
kupita kiasi, wengine wanawatishia
kuwafukuza kazi wakati mamlaka hayo hawana. Tuwahimize walimu kufanya kazi kwa
bidii na kuzingatia taratibu zinazotakiwa lakini tusipende kuwatwisha mizigo isiyoendana
na uhalisia.
Aliongeza kuwa suala la
kukuza elimu sio jukumu la mwalimu peke yake bali jamii wakiwemo viongozi, wazazi
na walezi katika maeneo yao wana sehemu kubwa kusaidia kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha
wanafunzi kufaulu.
“Wapo baadhi ya wazazi
ambao hawafuatilii maendeleo ya watoto wao kabisa, wapo wengine ambao bado
wanawafundisha watoto kuandika majibu ya uongo ili wasifaulu. Sasa hapa ni
lazima viongozi kama madiwani na wengine wajitahidi kuwaelimisha wazazi ili
waunge mkono juhudi za kuinua kiwango cha elimu”, alisema.
Alihitimisha kuwa Tume
ya Utumishi wa Walimu ina wajibu wa kuwaelimisha walimu ili wasijihusishe na
makosa ya kinidhamu katika utumishi wao na sio kwamba kazi kubwa ya Taasisi
hiyo ni kusubiri walimu watende makosa ili iwafukuze kazi.
No comments:
Post a Comment