HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 15, 2018

Wafanyabiashara Endeleeni kulipa Kodi:Dkt.Abbassi

Na Grace Semfuko-MAELEZO
 
Wafanyabiashara nchini wametakiwa kuendelea kulipa kodi na kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki za kukusanyia mapato (EFD) ili wasiingie katika migogoro isiyo ya lazima na serikali. 

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Idara ya habari Maelezo na msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbassi katika mahojiano maalum na redio Uhuru ya Jijini Dar es Salaa, kuelezea mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi cha miaka mitatu tangu iingie madarakani.

“Wafanyabiashara wale wanaokwepa kulipa kodi, tutawafikia, ni mkuhimu ulipe kodi ili iweze kufanya kazi za kuwahudumia watanzania, na kwa  mawakala wa kukusanya kodi wahakikishe wanaifikisha kodi hizo serikalini kwa wakati” alisema. 

Dkt Abbasi amesema Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Magufuli inafanya kazi kubwa ya kuhakikisha Watanzania wanapata maisha bora, hivyo ulipaji wa kodi ni muhimu sana ili fedha hizo ziwezeshe kupatikana kwa huduma bora zaidi kwa watanzania. 

Aidha  Dkt. Abbassi amewataka watendaji kwenye taasisi za umma kufanya kazi kwa weledi na kwa kujituma pia kuzingatia majukumu yao yaliyopo kwenye mikataba yao ya kazi ili kuleta ufanisi  kwenye taasisi zao. 

Alisema  Serikali haitasita kuwachukulia hatua za kinidhamu watendaji wote wa umma ambao hawawajibiki ipasavyo kwani wamekuwa ni mzigo kwa Serikali, na wanakwamisha jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Magufuli.

“Mmeona wenyewe juzi tu Mheshimiwa Rais amefanya maamuzi magumu lakini ni sahihi kabisa ya kuwaondoa baadhi ya watendaji wasiowajibika Serikalini,haiishii kwenye ngazi ya juu tu hii ni kwa kila mtendaji wa Serikali kuanzia ngazi za chini” alisema Dkt. Abbassi. 

Dkt.Abbasi alisema kuna mjadala mkubwa duniani unaendelea kuhusu maendeleo na nini maana ya kuwekeza, ambapo Tanzania imewekeza kwenye miradi mbalimbali ya maendeleo na  miundombinu pamoja na watu kwa maana ya watumiaji wakuu wa miradi hiyo.

Kuhusu elimu amesema serikali inatoa shilingi bilioni 23.85 kila mwezi ili kugharamia elimu kwenye shule za Serikali ikiwa ni mojawapo ya mkakati wa kuimarisha elimu nchini na hasa katika utekelezaji wa sera ya Serikali ya elimu bure kuanzia ngazi ya awali mpaka kidato cha nne.

Fedha hizo zinapelekwa moja kwa moja kwenya akaunti za shule badala ya kupelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya na Manispaa ambazo zilikuwa zikichelewesha fedha hizo kufika shuleni ama kutumiwa kwa matumizi yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

Pages