HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 23, 2018

Riadha, Baiskeli waonyeshana kazi Tamasha la Michezo Karatu

 Wanaume wakichuana katika mbio za kilometa 10 za Tamasha la 17 la Michezo na Utamaduni la Karatu lililofanyika jana mjini Karatu, Arusha.
 Wapanda baiskeli wakichuana katika mbio za umbali wa kilometa 60 wakati wa Tamasha la Michezo na Utamaduni la Karatu jijini Karatu Arusha.
Wanariadha wakike wakichuana katika mbio za kilometa tano za Tamasha la Michezo  na  Utamaduni la Karatu lililofanyika mjini Karatu, Arusha.
Mshindi wa mbio za Baiskeli kwa wanawake, Makirikiri Joseph, akiaonyesha manjonjo ya kuendesha baiskeli akiwa amebeba ndoo ya maji kichwani.
 
NA MWANDISHI WETU, KARATU

TAMASHA la 17 la Michezo Karatu (KSF), limefanyika mjini hapa jana huku ikishuhudiwa mchuano wa hali ya juu upande wa Riadha na Mbio za Baiskeli.

Kwa upande wa mbio za Km. 10 kwa wanaume ilishuhudiwa mchuano mkali kati ya Gabriel Geay wa Klabu ya Talent ya Arusha, Emmanuel Giniki wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), na Fabiano Sulle wa Polisi.

Katika mchuano huo, Geay aliibuka kinara akitumia dakika 30:03.37 akifuatiwa na Giniki 30:10.51, wakati nafasi ya tatu ikienda kwa Sulle aliyetumia dakika 31:06.91.

Kwa upande wa mbio hizo, Mwanariadha anayechipukia Francis Damiano wa klabu ya Rift Valley inayodhaminiwa na DStv ya mkoani Manyara, alipambana mbele ya wakali hao na kuibuka wa tano akitumia dakika 31:21.79 akitanguliwa nafasi ya nne na Marco Joseph wa Talent nafasi ya nne dakika 31:14.04.

Kwa upande wa wanawake Km. 5, mshindi Failuna Abdi wa Talent alishinda akitumia dakika 16:52.22 akifuatiwa na Natalia Elisante pia wa Talent dakika 17:40.54 na nafasi ya tatu Angelina Tsere wa JKT 17:51.07.

Mbio za Baiskeli, Waendesha Baiskeli wa Kanda ya Ziwa wakishiriki kwa mara ya kwanza tamasha hilo la michezo la Karatu, wamefanya maajabu baada ya kushika nafasi za kwanza kwa wanaume na wanawake.

Wakishangaza wengi, wakitumia baiskeli za kawaida lakini waliwagaragaza wapinzani wao, ambao wengi wao walitumia baiskeli rasmi za mashindano.

Mshindi wa kwanza kwa wanaume Km. 60, Masunga Duba kutoka mkoani Simiyu alishinda akitumia saa 1:31.46 akifuatiwa na Gerald Konda wa Shinyanga saa 1:36.12 huku nafasi ya tatu ikienda kwa mpanda baiskeli wa kimataifa Richard Laizer wa Arusha aliyetumia saa 1:36.18.

Laizer ndiye alikuwa bingwa mtetezi wa mashindano hayo, lakini alishindwa kuonesha cheche zake mbele ya wachezaji hao wa Kanda ya Ziwa walioshiriki kwa mara ya kwanza.

Kwa wanawake baiskeli Km. 30, Makirikiri Joseph kutoka Shinyanga alishinda kwa kutumia saa 1:12.20 akifuatiwa na Laurensia Ruzuba wa Mwanza aliyetumia saa 1:13.40 na nafasi ya tatu kwenda kwa Habiba Mathias kutoka Arusha aliyetumia saa 1:15.19.

Kwenye soka, bingwa aliibuka Serena FC ya Mbulumbulu huku mshindi wa pili ni Ghorofani FC ya Eyasi nafasi ya tatu ilichukuliwa na wenyeji Bodaboda FC ya Karatu.

Mpira wa Wavu, kwa wanaume timu ya Pentagon lishinda wakati mshindi wa pili ni KKKT Mbulu huku nafasi ya tatu ikienda kwa KKKT Karatu huku kwa wanawake bingwa ni Kirani ya Oldiani ikifuatiwa na KKKT Karatu huku KKKT Mbulu ikimaliza ya tatu.

Akizungumzia baada ya kumaliza mbio za baiskeli, Makirikiri Joseph alisema barabara iliyotumika ambayo sehemu kubwa ilikuwa ni ya changarawe ilikuwa ni rafiki kwake kwani ndiyo huwa wanazitumia zaidi huko kwao.

Kwa upande wake, Rais wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Gulam Rashid alisema tamasha hilo kimekuwa na mwitikio mkubwa na mwakani litaendelea kufanyika tena. Tamasha hilo liliandaliwa na Filbert Bayi Foundation (FBF) na kudhaminiwa na Olympic Solidarity (OS).

No comments:

Post a Comment

Pages