Naibu Waziri ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, akifurahia mabenchi 52 yaliyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya kupumzikia ndugu na wagonjwa wanaohudumiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), hafla ya makabidhiano ilifanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd na katikati ni Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura wa Muhimbili, Dk. Juma Mfinanga. (Picha na Francis Dande).
NA SALUM MKANDEMBA
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema inathamini mchango na misaada mbalimbali inayotolewa na Benki ya NMB kwa Sekta ya Afya nchini, kupitia Kitengo cha Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa wizara hiyo, Dk. Faustine Ndugulile, wakati akipokea msaada wa mabenchi 52 yenye thamani ya Sh. Milioni 10, yaliyotolewa na NMB kwa ajili ya kupumzikia ndugu na wagonjwa wanaohudumiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea msaada huo, Dk. Ndugulile alisema malengo ya serikali ni kuboresha miundombinu katika sekta ya afya, lakini ili kufanikisha hilo inahitaji misaada na michango ya wadau kama inavyofanywa na NMB.
Dk. Ndugulile alisema licha ya bajeti ya wizara yake kupanda mwaka hadi mwaka katika miaka 57 ya Uhuru wa Tanganyika, bado wizara yake na Serikali inahitaji na inathamini michango mbalimbali ya wadau na kuzitaka taasisi zingine kuiga mfano wa NMB.
“Mabenchi haya yatawasaidia sana ndugu wanaosindikiza wagonjwa, pia kwa wagonjwa wanaosubiri kuhudumiwa. Niwaombe kutanua wigo wa kuyafikia makundi mengine yenye uhitaji ndani ya wizara hii, katika hospitali zertu, zahanati zetu na vituo vya afya kote nchini,” alisema Dk. Ndugulile.
Kwa upande wake, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd, alisema benki yake kupitia CSR, inaguswa na changamoto zinaoikabili jamii, hususani katika sekta za afya, elimu na majanga na ndio maana ikatenga asilimia moja ya pato la mwaka kusaidia nyanja hizo.
Aliongeza ya kuwa, NMB inajisikia faraja inaposaidia sekta hizo na kuongeza kuwa ujenzi wa Taifa unawahitaji jitihada za wazawa, kwani si vema kusaidiwa kila kitu na wageni, huku akiahidi usaidizi zaidi wa changamoto hizo katika mwaka ujao wa fedha.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Muhimbili, Dk. John Rwegasha, aliipongeza NMB kwa namna inavyojitoa mara kwa mara kusaidia utatuzi wa changamoto zinazoikabili hospitali hiyo na kuwaomba kuendelea kuwasaidia bila kuwachoka.
Dk. Rwegasha alibainisha kuwa, msaada huo umekuja kwa wakati, kwani unaenda kujenga mazingira rafiki kwa wagonjwa na ndugu wanaowasindikiza wakati wakisubiri huduma na kumaliza adha ya kukosa sehemu sahihi ya kutulia na kupumzikia hospitalini hapo.
No comments:
Post a Comment