WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema taasisi binafsi na mashirika ya dini
yaendelee kuangalia namna ya kupanga gharama za huduma wanazotoa
zikiwemo za elimu na afya ili ziwiane na hali halisi ya vipato vya
wananchi.
“Hivi
sasa, Serikali kupitia vyombo mbalimbali inachukua hatua za makusudi za
udhibiti ili kuhakikisha Watanzania wanapata huduma zenye viwango,
ambapo baadhi ya wadau na wamiliki wanailalamikia Serikali kuwa
inawakandamiza na kuwawekea masharti magumu.”
Ameyasema
hayo leo (Ijumaa, Februari 22, 2019) wakati akizindua shule ya
Sekondari Jumuishi ya Mtakatifu Amachius Inclusive katika wilaya ya Hai
mkoani Kilimanjaro. Amezindua shule hiyo kwa niaba ya Rais Dkt. John
Magufuli.
Waziri
Mkuu amesema lengo la udhibiti huo ni kuimarisha viwango na ubora wa
elimu inayotolewa, hivyo ni muhimu kwa wadau wote kuzingatia sheria,
taratibu, kanuni na miongozo iliyowekwa na Serikali.
Amesema
utoaji wa elimu bora kwa Watanzania ni moja ya vipaumbele vya nchi
katika kuleta maendeleo na kufikia malengo ya Milenia 2025, Elimu kwa
wote (EFA) na Mkakati wa Kupambana na Kupunguza Umasikini Tanzania
(MKUKUTA).
Pia,
Waziri Mkuu amesema ili kuweza kufanikisha hayo wanahitaji sekta hiyo
kuwa bora, imara, inayokidhi mahitaji ya jamii kwa kuwapa vijana maarifa
na ujuzi wa kukabiliana na matatizo ya kijamii, kitaifa na kimataifa.
Akizungumzia kuhusu mafanikio ya sekta ya elimu, Waziri Mkuu amesemaSerikali
kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali imepata mafanikio
makubwa sana katika upatikanaji wa huduma za jamii ikiwemo elimu, afya
na maji.
”Hivi
sasa kila kijiji nchini kina shule ya msingi na ongezeko limefikia
idadi ya shule za msingi 17,659 zikiwemo zilizo chini ya Kanisa katoliki
204. Pia, tumejenga shule za sekondari katika kila kata, ambazo zipo
4,883 nchi nzima zikiwemo 266 zilizo chini ya kanisa katoliki.”
Amesema
idadi hiyo ya shule imesaidia kutoa fursa kwa wanafunzi wengi kupata
elimu katika ngazi mbalimbali nchini na kwa kuzingatia Ilani ya Uchaguzi
ya Chama cha Mapinduzi wanatekeleza mpango wa elimu msingi bila ada.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa Serikali inatoa kiasi cha shilingi bilioni 24.4
kila mwezi kwa ajili ya kughalamia mpango wa elimu msingi bila ada, kwa
lengo la kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kwenda shule anapata
fursa bila vikwazo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeongeza idadi ya wanufaika na Elimu
ya Juu kwa kuongeza bajeti ya fedha za mikopo kwa wanafunzi, ambapo kwa
sasa inatoa zaidi ya shilingi bilioni 483 kwa mwaka.
”Kwa
upande wa afya tunaendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma kwa kujenga
zahanati katika kila kijiji, kuimarisha vituo vya afya na ujenzi wa Hospitali 67 katika Halmashauri na Hospitali 4 za Rufaa kwenye Mikoa ambayo haikuwa na Hospitali za Rufaa. Upatakinaji wa dawa umeimarika kwa zaidi ya asilimia 90.”
Waziri Mkuu amesema licha yamikakati
waliyonayo na namafanikio wanayoyapata, Serikali inathamini sana
mchango wa sekta binafsi na taasisi za dini katika kuimarisha
upatikanaji wa huduma za elimu, afya, maji na miundombinu ya barabara.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amewataka wazazi na walezi kutowaficha ndani watoto wenye
mahitaji maalumu na badala yake wawapeleke shule kwa kuwa nao wanahaki
ya kupata elimu kama watoto wengine.
”Wakuu
wa wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri hakikisheni watoto wote wenye
mahitaji maalumu kwenye maeneo yenu wanapelekwa shule na wachukulieni
hatua wote watakaobainika wamewaficha watoto hao.”
Akiwa
shuleni hapo Waziri Mkuu ameshuhudia mmoja wa wanafunzi wa kidato cha
kwanz, Joseph Joachim ambaye hana mikono akiandika kwa kutumia vidole
vya miguu. ”Mwanafunzi huyu anandika muandiko mzuri kupita hata
wanaotumia mikono haya ni maajabu ya Mwenyezi Mungu.”
Awali,Mkuu wa shule hiyo Padri Patrick Asanterabi alisema ujenzi
wa shule hiyo hadi hivi sasa umepita katika awamu saba tangu kazi ya
ujenzi ilipoanza rasmi mwaka 2015. Kwa sasa shule inawanafunzi 74 huku
lengo ni kufikisha ni wanafunzi 500 itakapokamilika.
Alisema
ujenzi huo ulianza kwa tukio la kubariki kazi kwa ‘kupiga jembe la
kwanza’ lililofanywa na Mhashamu Askofu Mkuu Isaac Amani, wakati huo
akiwa Askofu wa Jimbo katoliki Moshi.
“Kuanzia
hapo, miundombinu mbalimbali ilijengwa ikiwemo, madarasa, vyoo,
mabweni, ukumbi wa shule, jengo la utawala, nyumba ya masista, jiko na
uwekaji wa mifumo ya umeme na maji.”
Alisema
shule imedhamiria kutoa elimu bora kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu
na wengine ili kuhakikisha wanakuwa na ulewa mzuri utakaowawezesha
kupata matokeo mazuri na kuendelea na masomo pamoja na kujitegemea.
Kwa upande wake,
Askofu Mkuu wa Jimbo la Arusha, Mhashamu Askofu Isaac Amani, ambaye
ndie muasisi wa shule hiyo alisema alipata wazo hilo baada ya mwanafunzi
mmoja wa kike aliyekuwa anasoma shule ya Mtakatifu Francis kumtembelea.
Alisema
mwafunzi huyo ambaye ni mlemavu wa macho alikuwa akisoma shule ya
msingi alimuuliza kuwa baada ya kumaliza watakwenda wapi kuendelea na
masomo kwani alisikia wenzao wanapangiwa shule ambazo miundombinu yake
si rafiki kwao ndipo akapata wazo la kuanzisha ujenzi wa shule hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, FEBRUARI 20, 2019
No comments:
Post a Comment