NA
MWANDISHI WETU
WANARIADHA wa Tanzania, Alphonce Simbu na Agustino Sulle
wamekuwa wa kwanza kufuzu kwa michezo ya Olimpiki itakayofanyika jijini Tokyo
Japan mwakani.
Wanariadha hao wamefanikiwa kukata tiketi hiyo jana nchini
Japan, baada yam kukimbia muda mzuri katika Mbio za Lake Biwa Marathon, ambazo
zinatambulika na zimepitishwa na Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF).
Katika mbio hizo zilizokuwa na ushindani wa hali ya juu kutoka
washiriki wa nchi mbalimbali, Simbu kutoka Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ),
na mshindi wa medali ya Shaba ya Dunia, alikamata nafasi ya sita akiandika
rekodi yake mpya, akitumia Saa 2:08.27.
Rekodi ya awali ya Simbu kabla ya jana ilikuwa ni Saa 2:09.10
aliyoiweka London Marathon.
Kwa upande wake, Sulle wa Klabu ya Taleny ya jijini Arusha, ambaye
anashikilia rekodi ya Taifa Marathon ya Saa 2:07.45 aliyoiweka Toronto Marathon
Canada mwaka jana, alishika nafasi ya 17 akitumia Saa 2:12.42.
Muda wa kufuzu kwa Olimpiki ambao unaanza kutambuliwa kuanzia
Januari mwaka huu ni Saa 2:14. kwa wanaume Marathon.
Katika mbio za jana Lake Biwa, Tanzania iliwakilishwa na
wanariadha watatu mwingine akiwa Gabriel Geay, ambaye alikwenda maalumu kama ‘Pace
Maker’.
Katika mbio hizo, mshindi wa kwanza aliibuka Salah
Eddine-Bounasr wa Morocco aliyetumia Saa 2:07.52 akifuatiwa na Asefa Tefera wa
Ethiopia 2:07.56 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Stephen Mokoka wa Afrika
Kusinia 2:07.58.
Akizungumzia matokeo
hayo, Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Wilhelm Gidabuday,
aliwapongeza wanariadha hao na walimu wao kwa mafanikio hayo na kwamba yamekuja
wakati muafaka.
Gidabuday, alisema RT chini ya Rais wake Anthony Mtaka na
Kamati nzima ya Utendaji, hivi sasa wako kwenye mikakati ya kuhakikisha mwaka
huu 2019 unakuwa ni wa kazi kutokana na kukabiliwa na matukio matatu makubwa
kimataifa kabla ya Olimpiki 2020.
“Kama mnavyofahamu, hivi sasa RT tunapata sapoti kutoka kwa
wadau mbalimbali kutokana na kuridhishwa na uwajibikaji wa wanariadha…Ni hivi
karibuni tumeingia makubaliano maalumu na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kutusapoti
katika maandalizi ya mashindano mbalimbali kuelekea Olimpiki Tokyo 2020 hivyo
kwa mwanzo huu wa vijana wetu tunaona umekuja wakati muafaka,” alisema
Gidabuday.
Katibu huyo, aliongeza kuwa ni mategemeo yao vijana wengi
zaidi watazidi kufuzu kwa mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwamo ya Dunia
Doha Qatar na Olimpiki Tokyo 2020.
No comments:
Post a Comment