HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 21, 2019

Vyombo vya habari vyatakiwa kuwajibika kwa wananchi wakati wa uchaguzi


Na George Binagi-GB Pazzo, BMG

Vyombo vya habari nchini Tanzania vimepewa changamoto ya kufanya kazi kwa weledi katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na Uchaguzi Mkuu kwa kuripoti habari zinazowasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.

Mkurugenzi wa taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa aliyasema hayo kwenye warsha ya kuwajengea uwezo viongozi wa vyombo vya habari na taasisi za uchaguzi katika kuangalia na kuripoti habari za uchaguzi, iliyofanyika jijini Dodoma kwa siku tatu kuanzia Machi 15, 2019.

Gasirigwa alisema waandishi wa habari/ vyombo vya habari wanapaswa kuzingatia sheria katika kutekeleza majukumu yao wakati wa uchaguzi ili kuhakikisha kunakuwa na uchaguzi wenye amani hivyo warsha hiyo itawasaidia wakati ambao Tanzania inaelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka huu pamoja na Uchaguzi Mkuu hapo mwakani.

Akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo, Makamu Mwenyekiti wa MISA Tanzania, wakili James Marenga alisema ipo haja vyombo vya habari kufanya kazi kwa kushirikiana vyema na mamlaka za uzimamizi wa uchaguzi hususani Tume ya Taifa ya Uchaguzi NEC hatua itakayosaidia kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza ikiwemo waandishi wa habari kuzuiliwa kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura.

“Jukumu la vyombo vya habari ni kuripoti kwa uwazi mchakato wote wa uchaguzi hivyo kuwazuia waandishi wa habari kuingia kwenye vyumba vya kupigia kura inaweza kuibua hofu kwa wananchi wakidhani hakuna uwazi kwenye uchaguzi huo” alisema wakili Marenga.

Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo iliyoandaliwa na MISA Tanzani kwa kushirikiana na Ubalozi wa Marekani, akiwemo Joyce Shebe kutoka Clouds Media Group walisema itawasaidia kutambua sheria mpya za vyombo vya habari na hivyo kufanya kazi kwa welezi katika kuripoti habari za uchaguzi, kutambua maswali sahihi ya kuuliza yatakayojibu kiu ya wananchi na hivyo kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura.
Mkurugenzi wa taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) tawi la Tanzania, Sengiyumva Gasirigwa akizungumza wakati wa warsha hiyo.
Wakili wa Mahakama Kuu Tanzania ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Wakili James Marenga akiwasilisha mada kwenye warsha hiyo.
Mmoja wa washiriki wa warsha hiyo akichangia mada.
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo.
Washiriki wakifuatilia kwa umakini warsha hiyo.
Baadhi ya viongozi wa vyombo vya habari Tanzania wakifuatilia warsha hiyo.
Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (V.O.A), Dk. Mwamoyo Hamza (katikati), akichangia mada kwenye warsha hiyo.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri Media, Deodatus Balile (kushoto), pamoja na Kaimu Msemaji wa Serikali, Zamaradi Kawawa (kulia) wakifuatilia kwa umakini warsha hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages