HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 21, 2019

WENYE TABIA YA KULA OVYO MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI KUCHUKULIWA HATUA

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilifungua Kongamano la Tatu la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani lililofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakili Kikwajuni Mjini Zanzibar.Baadhi ya Wakurugenzi na Wasaidizi wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akifuatilia hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.Baadhi ya Wana Kamati wa Jumuiya ya Zanzibar and Relief  Development Foundation (ZARDEFO) wakiwa makini kusikiliza Hotuba ya Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.Baadhi ya Wana Kamati wa Jumuiya ya Zanzibar and Relief  Development Foundation { ZARDEFO } wakiwa makini kusikiliza Hotuba ya Mgeni Rasmi kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan. Mwenyekiti wa Bodi ya Jumuiya ya Zanzibar and Relief  Development Foundation { ZARDEFO } Bwana Sleyum Mustafa Aboud akitoa salamu kwenye hafla ya uzinduzi wa Kongamano la Tatu la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu Wanawake wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Baadhi ya Waumini wa Dini ya Kiislamu Wanaume wakifuatilia hafla ya ufunguzi wa Kongamano la Tatu la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani. Mhadhiri  Mashuhuri wa masuala ya Dii ya Kiislamu wa Afrika Mashariki kutoka Mombasa Nchini Kenya Sheikh Iyzudiyn Alwi Akiwasilisha mada isemayo Ndoa ndio chanzo cha utu Wetu kwenye Kongamano hilo.Balozi Seif Kulia akimpongeza Mhadhiri  Mashuhuri wa masuala ya Dii ya Kiislamu wa Afrika Mashariki kutoka Mombasa Nchini Kenya Sheikh Iyzudiyn Alwi baada ya kumaliza kutoa mada yake iliyoelezea Ndoa ndio chanzo cha utu Wetu na kugonga nyoyo za waliohudhuria Kongamano hilo. (Picha na OMPR – ZNZ).

Na Othman Khamis Ame

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuuheshimu pamoja na kuutukuza Mwezi Mtukufu wa Ramadhani  kwa kutovumilia vitendo vyote vyote  vinavyokwenda kinyume na maadili ndani ya Mwezi huo.
Alisema tabia ya kula ovyo hadharani wakati wa mchana ndani ya mwezi huo pamoja na mambo mengine yanayoleta ushawishi wa kuwabughudhi waumini wanaokuwemo kwenye nguzo hiyo ya Funga inapaswa kuwepukwa vyenginevyo muhusika atakayeendeleza tabia hiyo atawajibika kwa kuchukuliwa hatua zinazostahiki.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akilifungua Kongamano la Tatu  la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani liloandaliwa na Jumuiya ya Zanzibar Relief and Development Foundation kwa kushirikiana na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Sheikh Idriss Abdulwakil Kikwajuni Mjini Zanzibar.
Aliwaomba Waumini wa Dini nyengine kuendelea na mfumo wao uliozoeleka wa kupata chakula na vinywaji majumbani mwao kitendo kinachoashiria upendo pamoja na uvumilivu wa kuheshimiana katika masuala ya kumuabudu Mwenyezi Muungu.
Alisema Ramadhani ni Mwezi wa kuchuma thawabu ukibeba neema nyingi na baraka ambapo waumini  wanahitaji kupata utulivu na amani  katika kutekeleza Ibada zao kwa kipindi hichi huku wakiusubiri Mwezi huo ili waweze kuonyesha Utii kwa Muumba wa vyote vilivyomo Duniani.
Balozi Seif  alieleza kwamba Falsafa ya Ramadhani iliyobeba umuhimu wa kusali sala za Jamaa, sala ya Tarawehe,visimamo vya Usiku, kuoneana huruna na kusaidiana, kutoa sadaka na Zaka ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa sio na Wanakongamano pekee bali hata kwa Wananchi  wote.
Aliwanasihi Waumini wa Dini ya Kiislamu na Wananchi wote waendelee kumshukuru Mwenyezi Mungu mara kwa mara kwa neema mbali mbali alizowajaalia ikiwemo Amani na Utulivu ili azidishe baraka  kwao kama alivyowaahidi katika Vitabu na Miongozo yake Takatifu.
Alisema bila ya neema hizo  hakuna jambo lolote lingeweza kufanyika akitolea Mfano uwepo wa Kongamano hilo lililokusanyisha Waumini kutoka maeneo mbali mbali Nchini Mjini na Vijijini ikiwemo Nchi jirani.
“ Kama tunavyoelewa kumshukuru Mola wetu kwa neema anazotujaalia ni jambo jema na Mola wetu ametuahidi kutuzidishia zaidi baraka za neema hizo”. Alisema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.
Akizungumzia Mada muhimu inayoelezea Ndoa chanzo cha Utu wetu iliyowasilishwa na Mwanafalsafa wa Dini ya Kiislamu kutoka Mombasa Nchini Kenya Sheikh Iyzudiyn Alwi, Balozi Seif  alisema ni maudhui muhimu kwa kuzingatia wakati huu  ambapo kuna ongezeko kubwa la talaka katika Jamii.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema bila shaka mafunzo hayo yanatoa fursa kwa Jamii kujifunza juu ya maisha sahihi ya ndoa kama yanavyofundishwa kwenye Kitabu Kitukufu cha Quran Karim na Mafundisho ya Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Mtume Muhammad {SAW}.
Alisema bila ya ndoa utu wa Mwanaadamu haukamilii kwa vile hukosa utulivu wa moyo jambo ambalo limepewa uzito na Mwenyezi Mungu aliyowajengea daraja ya juu Wanaadamu mbele ya viumbe wengine kwa kuoana kisheria kwa lengo la kulinda nasaba.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar kwa kuendesha mafunzo ya maadili ya ndoa kwa ajili ya Wanandoa watarajiwa pamoja na wale ambao tayari wameshaingia kwenye Sunna hiyo inayogeuka kuwa Wajibu kutokana na uzito wake.
Kwa upande wa Sekta ya Biashara ndani ya Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Balozi Seif aliwasihi Wafanyabiashara kuacha hulka ya kupandisha kiholela bei za bidhaa muhimu zinazotumika katika Mfungo wa mwezi wa Ramadhani  hasa vile vyakula vya nafaka.
Balozi Seif alisema Wafanyabiashara lazima wazingatie Falsafa ya Ramadhan inayowasisitiza Waumini na Wananchi wakiwemo pia Wafanyabiashara kuendelea kuhurumiana na kusaidiana ndani ya Mwezi huo pekee uliobeba baraka.
Akitoa Taarifa ya Kongamano la Tatu la kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Zanzibar Relief  and Development Foundation { ZARDEFO } Bwana Ali Mohamed  Haji alisema Taasisi hiyo itaendelea kusimami masuala mbali mbali yanayostawisha Jamii Nchini.
Bwana Ali Mohamed alisema mbali ya Taasisi hiyo kusimamia masuala ya Elimu lakini pia katika kutanua majukumu yake imekusudia kuendesha miradi Minne mkubwa itakayotoa nafasi ya kusaidiana na Serikali katika mapambano ya kupunguza wimbi la ukosefu wa ajira.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kisasa, Mradi wa Uvuvi, Kilimo cha Kisasa pamoja na uendelezaji wa Miradi ya ujasiri Amali ikilenga kuwainua zaidi Vijana Kiuchumi.
Hata hivyo Bwana Ali Mohamed alisema ipo changamoto ya ukosefu wa ushirikiano kwa baadhi ya Taasisi na hata Watu binafsi zinazochangia kuzorotesha harakati za Taasisi hiyo katika kustawisha Maisha ya Wananchi hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Akimkaribisha mgeni Rasmi kwenye Kongamano hilo la Kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Mh. Khamis Juma Mwalimu alisema Kongamano hilo ni muhimu  kwa vile linatoa fursa kwa Waumini na Wananchi kukumbushana juu ya wajibu wao.
Warizi Khamis alisema wapo baadhi ya Watu hasa Vijana huukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan  kwa kuandaa mambo yanayochukiwa na Mwenyezi Mungu ikiwemo safari za starehe zenye kuambatana zaidi na vitendo vilivyo nje ya maadili na Tamaduni za Kiislamu.
Akiwasilisha mada isemayo Ndoa ndio chanzo cha utu Wetu Mhadhiri  Mashuhuri wa masuala ya Dii ya Kiislamu wa Afrika Mashariki kutoka Mombasa Nchini Kenya Sheikh Iyzudiyn Alwi alisema sifa zote nzuri za Mwanaadamu chimbuko lake hutokana na Utu.
Sheikh Alwi alisema utu unakamilika kutokana na chimbuko la ndoa lilosheheni uvumilivu, kusikitikiana kwenye matatizo, kuepuka ugomvi kutokana na busara pamoja na kustahamiliana.
Alisema kwamba maumbile ya kawaida ya wanaadamu yanaambatanisha jinsia mbili zilizofungamana na mfumo wa  ndoa halali  iliyobeba sheria na taratibu zote za kidini ikilenga kuleta utulivu kwa Wanaume baada ya mahangaiko yake ya kila siku ya Kimaisha.
Alisisitiza kwamba nusu ya Dini yote iko kwenye ndoa inayosukuma mafanikio makubwa nje ya familia katika mauala mazito hasa ya kuwaongoza Waumini wengine.

No comments:

Post a Comment

Pages