WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa ameuagiza uongozi wa bodi ya KADCO uhakikishe unaweka mabango ya
kielektroniki yenye kuonesha vivutio vya utalii kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa
wa Kilimanjaro (KIA).
“KADCO na
Wizara ya Maliasili na Utalii, shirikianeni kuweka utaratibu wa
kutangaza vivutio vyetu vya utalii hasa wanyama kwenye viwanja vyote vya ndege.
Tunazo mbuga, milima, fukwe za bahari na ngoma za makabila mbalimbali, wekeni
mabango yanayobadilisha picha.”
“Screens zenye wanyama wanaobadilikabadilika
zinaleta mvuto lakini pia ni fursa ya kutangaza vivutio vyetu. Nimezunguka humu
ndani, kuta zote ni nyeupe tu, tumieni fursa hiyo kutangaza tamaduni zetu na
vivutio tulivyonavyo," Waziri Mkuu alimweleza Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Kilimanjaro Airports Development Company (KADCO), Mhandisi Christopher
Mukoma.
Alitoa agizo hilo
jana mchana (Jumamosi, Aprili 27, 2019) wakati akikagua miundombinu ya uwanja
wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) mara baada ya kuwaaga watalii 274 kutoka Israeli
wanaowawakilisha wenzao 1,000 walioondoka nchini jana kurejea kwao.
Akiwa uwanjani hapo,
Waziri Mkuu alikagua eneo la mapokezi, sehemu ya abiria wanaoondoka na
wanaowasili, sehemu ya uhamiaji, mashine za kukagua mizigo ya wanaoondoka na
wanaowasili, sehemu za kutolea huduma na maduka.
Pia alimwagiza Mrakibu
Mwandamizi wa Uhamiaji kwenye kiwanja hicho cha ndege, Bw. Filbert Ndege
awasiliane na makao makuu yake ili waangalie uwezekano wa kuongeza madirisha ya
kutolea huduma za uhamiaji (counters) ili huduma hiyo itolewe kwa
kasi zaidi.
“Angalieni cha
kufanya, ikibidi eneo hili lipanuliwe na counters
nyingine ziongezwe ili kufast-track utoaji wa huduma hasa msimu ambao
watalii wengi huingia nchini.”
Pia aliwataka KADCO
waboreshe eneo la maegesho ya magari kwa kufanya upanuzi na kujenga maturubai
ya vivuli (shades) ili kuyakinga na jua kali magari ya wateja.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, APRILI 28, 2019.
No comments:
Post a Comment