HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

April 21, 2019

WAZIRI MKUU AITAKA PSSSF IONGEZE MAKUSANYO

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka menejimenti ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ijizatiti na kuweka mbinu mpya za kuongeza makusanyo.

Ametoa agizo hilo leo jioni (Alhamisi, Aprili 18, 2019) wakati alipokutana na menejimenti ya mfuko huo kwenye kikao kilichofanyika ukumbi wa mikutano wa PSSSF jijini Dodoma. 

Waziri Mkuu ambaye aliamua kutembelea ofisi za mfuko huo ili afahamiane na menejimenti hiyo, amesema amepokea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu na kubaini kuwa ukusanyaji wa michango hauridhishi. 

“Mfuko huu ni wa tofauti na wa NSSF kwa sababu umeunganisha mifuko mingine ya GEPF, PSPF, LAPF na PPF. Mifuko yote hii ilikuwa na malengo na majukumu yake ya awali, lakini sasa imeunganishwa kwa hiyo jukumu letu ni moja,” amesema.

“Natambua mna kazi kubwa ya kusajili wanachama wapya lakini pia tunayo kazi ya kuwafikia wanachama wa zamani ambao tumewachukua kutoka mifuko mingine na kuhakikisha kuwa wanaingizwa katika mfuko mpya,” amesisitiza.

“Napenda kusisitiza kuwa jukumu la kukusanya michango ni la muhimu sana. Ni lazima mjue wastani wa makusanyo kwa mwezi ni kiasi gani, na kama zimepungua, ni kwa kiasi gani na pia mtafute ni kwa nini zimepungua,” amesema.

Ameitaka menejimenti hiyo pia ijiridhishe juu ya uhakiki wa mali walizorithi kutoka mifuko mingine na izitambue ziko katika hali gani. “Menejimenti peke yenu hamuwezi kufuatilia mali zote, kwa hiyo wapeni hiyo kazi wajumbe wa Bodi, wagawane maeneo ili waende kuzitathmini hizo mali na kisha nipate hiyo taarifa,” amesema.

Mapema, akiwasilisha taarifa ya utendaji wa mfuko huo kuanzia Agosti Mosi 2018 hadi Machi 31, 2019, Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Hosea Kashimba alimweleza Waziri Mkuu kwamba majukumu makuu wa mfuko huo ni kusajili wanachama, kukusanya michango, kuwekeza na kulipa mafao kwa wanachama.

Alisema baada ya kuunganishwa kwa mifuko, uandikishwaji wa wanachama uliendelea ambapo hadi kufikia Machi 2019, jumla ya wanachama wapya 7,575 walikuwa wamesajiliwa.


“Hapo awali mfuko ulikuwa na wanachama 962,871. Kati ya hao, wanachama 279,564 wanatoka sekta binafsi ambao wamehamishiwa NSSF. Hadi kufikia Machi 31, 2019, mfuko ulikuwa na jumla ya wanachama 750,943 ambao ni watumishi wa umma ikijumuisha na wanachama 67,636 waliohamia kutoka NSSF,” alisema.

Kuhusu ukusanyaji wa michango, Bw. Kashimba alisema moja ya jukumu la mfuko ni kukusanya michango na tangu Agosti 2018 hadi Machi 2019, mfuko huo ulikuwa umekusanya jumla ya sh. bilioni 928.31 ikilinganishwa na lengo la lililowekwa la kukusanya sh. trilioni 1.05 sawa na asilimia 88.62.

Kuhusu malipo ya mafao, Bw. Kashimba alisema katika kipindi kilichoishia Machi 31, 2019, mfuko huo umelipa mafao ya jumla ya sh. trilioni 1.65.

Alisema mfuko huo hivi sasa una wafanyakazi 839 ambao kati yao, wanaume ni 470 na wanawake ni 369.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi, (OWM – Sera, Uratibu, Bunge na wenye Ulemavu), Bibi Jenista Mhagama.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
 41193 – DODOMA,                      
ALHAMISI, APRILI 18, 2019

No comments:

Post a Comment

Pages