WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watalii kutoka
Israel wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania pindi wakirudi huko kwao.
Ametoa wito huo leo mchana (Jumamosi, Aprili 27,
2019) kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) wakati akiwaaga watalii 274
walioondoka nchini leo mchana kurejea kwao.
Watalii hao ni miongoni mwa watalii 1,000
waliowasili nchini tangu Aprili 20, mwaka huu na kutembelea maeneo kadhaa ya
vivutio kwenye ukanda wa Kaskazini.
Kundi la kwanza liliondoka jana usiku, la pili leo
mchana, la tatu litaondoka leo saa 10 jioni na la mwisho litaondoka leo saa 2
usiku.
Waziri Mkuu amewaomba watalii hao wapange muda wao
na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea mbuga nyingine za ukanda
wa Kusini pamoja fukwe nzuri za Zanzibar.
"Tumefarijika sana na ujio wenu na tunaamini
mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. Tunazo mbuga nyingine za
Rubondo, Katavi, Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za Zanzibar na mlima
Kilimanjaro," amesema.
Pia amewashukuru mawakala wa utalii nchini pamoja na
Mkurugenzi wa kampuni wakala wa utalii ya Another World kutoka Israel Bw. Carmel
Shlomo kwa kuamua kuitangaza Tanzania kama kivutio namba moja cha utalii barani
Afrika.
Kwa
upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla aliwashukuru
watalii hao kwa kuamua kuitembelea Tanzania licha ya kuwa wangeweza kwenda
maeneo mengine yaliyo jirani na Israel.
"Natambua uchovu mlionao sababu ya urefu wa
safari kutoka Israel hadi hapa, lakini nawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuja
Tanzania katika kipindi hiki ambacho tunafanya maboresho kwenye sekta ya utalii
ili tuweze kutoa huduma bora zaidi," alisema.
Alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii na hii
inawezekana kwa sababu iliamua kutenga zaidi ya robo ya ardhi yake kwa ajili ya
mbuga na hifadhi za taifa za wanyama.
Pia alizishukuru kampuni za utalii za Tanzania na
Israeli kwa kushirikiana kuleta watalii wengi kiasi hicho. Alizitaja kampuni hizo
kuwa ni Excellent Guides, Mauly Tours and Safaris, Matembezi, Leopard Tours and
Safaris, African Queen Adventures na TAWISA zote za kutoka Tanzania. Kamuni za
kutoka Israeli ni Another World, My Trip, Camel na Safari Company.
Kwa
upande wao, baadhi ya watalii kutoka Israel wamesema wamevutiwa na waliyaona hapa
nchini na wameahidi kurudi tena ili watembelee vivutio vingine zaidi.
Bibi Naomi Peer Moscovich na mabinti zake Dana na
Lihi wamesema wamevutiwa na wingi wa wanyama waliowaona lakini pia wameguswa na
ukarimu wa watu waliokutana nao.
"Tunaondoka na neno moja kubwa nalo ni kwamba
hatutaisahau Tanzania (we say Unforgettable Tanzania) na tutarudi tena hivi
karibuni," alisema Dana Peer Moscovich ambaye ni dada yake Lihi.
Hafla ya kuwaaga watalii hao ilihudhuriwa pia na Mwenyekiti
wa Bodi ya Utalii nchini, Jaji Thomas Mihayo, Katibu wa Wizara ya Maliasili na
Utalii, Adolf Mkenda na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha. Mama Anna
Mghwira na Bw. Mrisho Gambo.
IMETOLEWA
NA:
OFISI
YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI,
APRILI 27, 2019.
No comments:
Post a Comment