Hii ni baada ya jana
usiku kutoka nyuma kwa mabao 2-0 dhidi ya Ajax Amsterdam ya Uholanzi, kisha
kushinda kwa mabao 3-2 na kuing’oa Ajax kwa sheria ya bao la ugenini. Pambano la
kwanza baina yao, Ajax iliilaza Spurs 1-0. Iwapo Arsenal na Chelsea zitafuzu
fainali ya Europa League leo usiku, basi England itakuwa nchi ya kwanza Ulaya
kuingiza timu nne katia fainali mbili kubwa.
Lucas Moura akiruka juu kushangilia moja ya mabao yake matatu aliyoifungia Tottenham. Picha na Daily Mail
Lucas Moura wa Tottenham katikati akishangilia bao lake la tatu lililoipeleka timu yake fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya jana usiku
Matthijs de Ligt wa Ajax akiruka juu kumzidi Dele Alli wa Tottenham na kuifungia bao la uongozi. Picha na Daily Mail
Shangwe la ushindi na kutinga fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Daily Mail
Wachezaji wa Tottenham wakishangilia ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ajax, uliowapa nafasi ya kutinga fainali Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Daily Mail.
AMSTERDAM, UHOLANZI
ENGLAND,
huenda ikawa nchi ya kwanza Ulaya kuingiza timu nne katika fainali mbili za
michuano mikubwa ngazi ya klabu barani humo, hii ni endapo Arsenal na Chelsea
zitachanga vema karata zao katika mechi za marudiano nusu fainali Europa League
leo usiku.
Tayari
Tottenham Hotspur ya London, imeungana na Majogoo wa Jiji Liverpool katika
fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UCL 2018/19), baada ya jana usiku kufanya ‘comeback
ya kibabe,’ ikitoka nyuma kwa mabao 2-0 ya Ajax Amsterdam kipindi cha kwanza na
kushinda 3-2.
Ulikuwa
ni muendelezo wa maajabu ya soka, yaliyotokea saa 24 tu tangu Liverpool
walipowababua FC Barcelona kwa mabao 4-0 na kupindua matokeo ya mechi yao ya
kwanza wa mabao 3-0 dimbani Camp Nou, Barcelona nchini Hispania.
Katika
nusu fainali ya pili jana, Tottenham, ikiwa na jeraha la kipigo cha bao 1-0
nyumbani, iliifuata Ajax Amsterdam ya Uholanzi kinyonge, hali iliyowafanya
kuanza pambano kinyonge na kukubali kipigo cha mabao 2-0 ndani ya dakika 35,
matokeo yaliyodumu hadi filimbi ya mapumziko.
Mabao
ya Ajax katika dakika 45 za kwanza yalifungwa na Matthijs de Ligt mapema dakika
ya tano, kabla ya Hakim Ziyech kuipa Ajax bao la pili dakika 30 baadaye, na
kuibua shangwe kuu miongoni mwa mashabiki 53,285 kwenye dimba la Johan Cruiyff
Arena, jijini Amsterdam.
Kipindi
cha pili Totenham walikuja kivingine na Mbrazil Lucas Moura akafanya maajabu
yake, baada ya kufunga mabao matatu ‘hat trick,’ na kuwapa Spurs ushindi wa
mabao 3-2 na kuipeleka fainali yao ya kwanza kwa sheria ya bao la ugenini,
kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni 3-3.
Moura
alifunga mabao yake katika dakika za 55 (pasi ya Dele Alli), dakika ya 59 (pasi
ya Danny Rose) na kuhitimisha ushindi dakika ya 90+6 (pasi ya Alli na
kuiwezesha Spurs kukata tiketiya kwenda Estadio Wanda Metropolitano, jijini
Madrid, Hispania itakopigwa fainali Juni 1.
Macho
na masikio ya Waingereza leo yanaelekezwa Hispania, ambako Arsenal walioshinda
kwa mabao 3-1 katika mechi ya nyumbani Emirates, wanarudiana na Valencia kwenye
viunga vya Mestalla, huku jijini London, Chelsea wakiwakaribisha Eintracht
Frankfurt ya Ujerumani baada ya sare ya 1-1.
Wakati
Arsenal watakuwa wakiwania ushindi ama sare ili kukata tiketi ya kwenda fainali
mjini Baku, Azerbaijan, Chelsea wao watakuwa wakipigania sare tasa ama ushindi
ili kuzalisha fainali ya Waingereza unayoweza kuiita ‘London Derby’ kutokana na
upinzani wa klabu hizo za mji mmoja.
Iwapo
Arsenal na Chelsea zitafanikiwa kutinga fainali ya Europa League, England
itakuwa nchi ya kwanza kuingiza timu zote nne katika fainali mbili za michuano
ya klabu Ulaya, lakini iwapo moja wapo itateleza, basi England inaweza kuingiza
timu tatu katika fainali mbili.
· Kumbukumbu zinaonyesha ya kuwa, mwaka 1980, Ujerumani
iliingiza timu za Eintracht Frankfurt na Borussia Monchengladbach katika
fainali ya UEFA Cup, huku timu nyingine ya nchi hiyo, Hamburg ikitinga fainali ya
Europian Cup na kuumanana Nottingham Forest ya England.
· Mwaka 1990, ni mwaka mwingine ambao nchi moja
iliingiza timu tatu katika fainali mbili za michuano ya klabu Ulaya, baada ya
Juventus na Fiorentina kuumana katika fainali ya Wataliano watupu ya UEFA Cup, huku
AC Milan nayo ikitinga fainali Ligi ya Mabingwa.
· Miaka minane baadaye (1998), Juventus ilitinga
fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku klabu zingine mbili za Serie A, Inter
Milan na Lazio, zikitinga na kuumana katika fainali ya UEFA Cup.
· Je England itaingiza timu nne fainali, au itaangukia
kuwa nchi tatu Ulaya kuingiza timu tatu katika fainali mbili za michuano
mikubwa barani Ulaya? Ni jambo la kusubiri na kuona na majibu yatapatikana leo
usiku baada ya Arsenal na Chelsea kushuka viwanjani.
Kikosi
cha Ajax katika mfumo wa 4-2-3-1 na
alama za ubora wao mchezoni: Onana 5; Mazraoui 6, Blind 6, De Ligt 7;
Tagliafico 6; Schone 6.5 (Veltman 58, 6), De Jong 7; Ziyech 8.5, Van de Beek
6.5 (Magallan 90), Tadic 7.5; Dolberg 5 (Sinkgraven, 67, 6).
Kikosi
cha Tottenham katika mfumo wa 4-2-3-1 na
alama za ubora wao mchezoni: Lloris 7; Trippier 5.5 (Lamela 81), Vertonghen 7,
Alderweireld 6.5, Rose 7.5 (Davies 83); Sissoko 8, Wanyama 5 (Llorente 46, 7);
Eriksen 6, Alli 7, Son 7; Moura 9.5.
Daily
Mail
No comments:
Post a Comment