Na Janeth Jovin
ASASI
300 za Kiraia nchini zimependekeza kusitishwa kwa mchakato wa muswada
wa mabadiliko ya sheria zinazohusu Asasi za kirai kwa kuwa umekuja kwa
hati ya dharura na haukuwashirikisha wadau.
Asasi
hizo zimesema wadau wanapaswa washirikishwe vya kutosha katika mchakato
wa muswada huo ili kupata maoni yao na endapo muswada huo ukipitishwa
bila kuwashirikisha watakwenda kuupinga mahakamani kwani athari zake ni
kubwa.
Akisoma tamko la
asasi hizo jijini Dar es Salaam juzi, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa
Watetezi wa Haki za Binadamu nchini (THRDC), Onesmo Olengurumwa, alisema
muswada huo uliopelekwa bungeni kama ukipitishwa na kuwa sheria basi
utakwenda kuua asasi za kiraia zilizopo nchini.
Alisema
muswada huo uliowasilishwa hivi karibuni bungeni kwa hati ya dharura
umezua sitofahamu na taharuki kwa azaki ambao ni walengwa wakuu kwenye
muswada huo.
"Miongoni
mwa sheria hizo ni sheria ya mashirikika yasiyo ya kiserikali ya mwaka
2002, sheria ya Jumuiya za kijamii, sheria ya mabaraza ya wadhamini na
sheria ya makampuni ya mwaka 2002. Sheria hizi ni miongoni mwa sheria
kuu zinazoongoza asasi za kiraia nchini," alisema.
Olengurumwa
alisema uchambuzi walioufanya na asasi za kiraia zaidi ya 170 endapo
muswada huo ukipitishwa utaleta changamoto nyingi katika utekelezaji na
uendeshaji wa azaki.
Alisema
miongoni mwa changamoto hizo ni kuminya kwa uhuru wa azaki nchini
kinyume na katiba pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo
Tanzania imeridhia.
Alisema
msajili amepewa mamlaka makubwa bila kudhibitiwa ya namna ya kusimamia
azaki ikiwa ni pamoja kufuta usajili wa azaki pasipo kufuata utaratibu
wa kisheria.
Naye
Mkurugenzi wa Taasisi ya Usawa kwa Wasichana (EFG), Jane Magigita,
alisema kutokana na changamoto walizoziona ni vizuri bunge likafanya
maboresho na kufuta vipengele vinavyoathiri azaki za nchini.
"Tunawaomba
wabunge kuusoma kwa umakini na kuuelewa muswada huu ili watakapokuwa
ndani ya bunge watoe mapendekezo ya kurekebisha vipengele vyote
vinavyoathiri azaki nchini," alisema
Magigita
alisema wanaomba muswada huo uondolewe kwenye hati ya dharura na
kushirikishwa katika hatua zote ikiwa ni pamoja na kukusanya maoni yao
kutoka kwa wadau mbalimbali.
No comments:
Post a Comment