HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 21, 2019

VAT YAKWAMISHA UJENZI WA STENDI MPYA YA MABASI

Na Janeth Jovin

HALMASHAURI ya jiji la Dar es Salaam imesema moja ya changamoto wanayokumbana nayo katika ujenzi wa mradi wa Stendi mpya ya Kisasa ya Mabasi ni kodi ya ongezeko la thamani (VAT) hali ambayo imesababisha vifaa vingi vikiwemo vya ujenzi kukwama bandarini.


Hayo yamebainishwa leo na Mkurugenzi wa jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, mbele ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sulemain Jafo, wakati akitoa maelezo ya mradi.

Waziri Jafo leo amefanya  ziara ya kukagua ujenzi wa mradi huo ili kujionea umefikia wapi pamoja na barabara zilizopo chini ya mradi wa Maendeleo ya Jijini Dar es Salaam (DMDP).

 Amesema Januari 18, mwaka huu Serikali Kuu iliwapatia kiasi cha Sh bilioni 50.9 bila VAT,  mkandarasi alianza kazi lakini kufikia Juni 19 mwaka huu wamekumbana na changamoto ya VAT.

Liana amesema amekuwa akifuatilia  suala hilo hadi hazina mkoani Dodoma  lakini mpaka sasa amekwama.

"Wiki iliyopita nilijulishwa kuwa kamati imeshakaa na kuidhinisha, hivyo ucheleweshaji huo endapo mkandarasi akiruhusiwa kwenda kununua vitu kuna uwezekano asirudishiwe fedha zake.

“Mheshimiwa Waziri tumesubiri sana tunaomba utusaidie tena katika suala hilo maana tumekwama na changamoto nyingine ilikuwa ya mvua kunyesha ilitusumbua sana lakini hadi sasa tumefikia asilimia 20 ya kazi hii ya ujenzi. VAT ikishughulikiwa mapema itasaidia hata kumaliza kabla ya muda,” alisema.

Akijibu hoja hiyo, Waziri Jafo amesema tayari alishamueleza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuhusiana na watu wake kukwama katika ujenzi kuhusiana na suala la VAT.

“Sio mradi huu tu umekwama miradi yote ya DMDP imekwama ninaimani kuwa Dk. Mpango atakwenda kulishughulikia kwani nilishamuambia na nimeandikia barua kwa kuwa Rais John Magufuli ametoa fedha hatupo tayari kuona unachelewa huu mradi,” alisema Jafo

 Aidha, Jafo amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuongeza kasi katika ujenzi huo na hataki kusikia kisingizio cha mvua kimewakwamisha.

“Huu mradi mpo nyuma kwa asilimia nane sitaki kusikia mvua mkandarasi kama watu wanajenga baharini baharini ni kuna maji mbona wanajenga,” alisema

“Hii miradi ni ya pekee na ndio maana Rais John Magufuli aliamua kutoa Sh bilioni 268.75 haijawahi kutokea ni kwa mara ya kwanza zamani ilikuwa jiji linachukua mikopo kwa benki za kibiashara,” alisema

Amesema Rais Magufuli alitoa Sh bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi huo wa kituo cha mabasi, hivyo ameridhindwa na utendaji kazi na kuwataka kukamilisha ndani ya muda.

Aidha, amemuagiza Mshauri Mwelekezi kuhakikisha anasimamia vizuri mradi huo na pasijitokeze kwa dosara ya aina yoyote.

“Ndio maana nilikuwa nakuuliza maswali mengi kuhusiana na huu mradi nataka kila kitu uwe unakijua wewe, mkandarasi anaweza kufanya vitu vidogo ili apate faida nataka mambo yaende vizuri hizi Sh bilioni 50 ni nyingi,” alisema

Amesema Stendi hiyo itakuwa kubwa na ya kisasa, hivyo ifikapo Septemba mwakani iwe imekamilka kabla ya kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Mimi ninachotaka kabla ya kuingia katika Uchaguzi Mkuu tumuite Rais Magufuli kuja kufungua huu mradi lengo ni watanzania waje kuona manufaa ya huu mradi,” amesema Jafo.

“Hii barabara hadi wataalamu wangu mmeisahau mmepata tabu kufika nilikuwa nawaangalia tu kwa nini mmenipoteza kufika hapa. Wataalamu wangu msipojua hizo barabara hamuweezi kujua changamoto za wananchi wanazozipata,” alisema

No comments:

Post a Comment

Pages