HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 27, 2019

JWTZ latoa tamko kali kwa vijana waliofanya udanganyifu

Na Janeth Jovin

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ)  limebaini kuwepo kwa udanganyifu wa hali ya juu katika zoezi la uandikishwaji wa vijana kujiunga na  Jeshi unaoendelea katika mikoa yote nchini na visiwani Zanzibar hali iliyowalazimu kuanza kupitia upya vijana wote walioandikishwa kote nchini.

Hayo yamebainishwa jijini Dar es Salaam leo na Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JWTZ, Luteni Kanali Gaudence Ilonda (pichani), wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu changamoto hizo zilizojitokeza wakati wa uandikishwaji.

Ilonda amesema kuwa moja ya changamoto iliyojitokeza ni idadi kubwa ya vijana kujiandikisha katika mikoa tofauti na ile wanayoishi hali ambayo amesema ni shindikizo ambalo mtoto amelipata kutoka kwa wazazi wao pamoja na viongozi.

"Wingi huo wa vijana wanaotoka  mikoa mingine na kwenda kwenye usa umesababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya vijana katika mikoa yao husiku ambao wamenyimwa fursa mwenyewe,".alisema.

Alisema kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wakipeleka majina ya vijana katika Makao makuu ya Jeshi la kujenga taifa na Mikoani kwa malengo ya kupata nafasi hizo kwa urahisi zaidi huku akieleza kuwa jeshi hilo halitoi ajira bali linawaandaa vijana hao kuwa wazalendo na viongozi bora kwa baadaye.

"Wapo viongozi na wanajijua ambao wamekuwa wakileta majina 10 hadi 20 ya vijana wao ii waweze kupata nafasi katika jeshi la wananchi, huku ni kujitengenezea kikosi kwa matumizi yao binafsi kwa baadaye jambo ambalo ni kinyume na kanuni za jeshi hilo" ameeleza Luteni Ilonda.

Aidha amesema kuwa changamoto nyingine katika zoezi hili la uandikishwaji ni udanganyifu wa vyeti vya elimu,vya kuzaliwa kwa kudanganya umri na afya pamoja na utapeli wakati wa uandikishwaji ambapo wazazi na walezi huombwa fedha ili kuweza kupata nafasi hizo.

"Vijana hawa kuna watu wanawasaidia kughushi vyeti hivyo basi niwahakikishie kila aliyefanya makosa atachukuliwa hatua ikiwamo ya kufunguliwa mashtaka mahakaani, ila kutokana na udanganyifu huu tutapitia upya majina haya tutawaita na kupimwa upya afya zao, " amesema Luteni Ilondo.

Vilevile amesema kuwa kufuatia dosari hizo ambazo hawataweza kuzifumbia macho Jeshi la kujenga Taifa kwa kushirikina na Jeshi la wananchi, mamlaka ya vitambulisho vya taifa (NIDA), Wizara ya elimu, Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) pamoja na mamlaka nyingine watashirikiana katika zoezi kabambe la kupitia upya vijana wote walioandikisha kote nchini pamoja na kupitia nyaraka na vyeti vyote kwa lengo la kupata vijana halali, watanzania, wenye afya na wanaotoka maeneo husika.

Amesema lengo la kuwapata vijana hao ni  ili waweze kuingia katika jeshi hilo na kupata mafunzo ya uzalendo, umoja, weledi, upendo na kujali mali za umma.

Luteni Ilonda amesema kuwa kwa watakaobainika wameshiriki katika udanganyifu huo kwa namna yoyote ile watakamatwa na kufunguliwa mashtaka na hakuna atakaye fumbiwa macho na hata wale waliotumia dhamana vibaya hawatastahimiliwa.

Hata hivyo  amewataka wananchi kufuata taratibu za uombaji wa nafasi hizo ambazo sifa za kujiunga zimebandikwa katika maeneo ya Wilaya na ofisi husika huku akiwataka vijana wanaojiunga na jeshi kuelewa kuwa hiyo sio tiketi ya ajira jeshini au serikalini bali ni sehemu ya kujifunza uzalendo na kuwa viongozi Bora wa baadaye.

No comments:

Post a Comment

Pages