Meneja wa Mradi wa Uanzishaji Miundombinu ya Upatikakanaji Taarifa za Ardhi
kutoka nchini Korea Hooyoung So akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo
katika ofisi za Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi zilizopo eneo la
Mtumba Jijini Dodoma tarehe 13 Juni 2019. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Ardhi Dorothy Mwanyika.
Na
Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dorothy Mwanyika amezindua mradi wa
Uanzishaji Miundombinu ya Upatikanaji Taarifa za Ardhi nchini.
Uzinduzi wa mradi huo
umefanyika katika ofisi za Wizara eneo la Mtumba jijini Dodoma na kuhusisha Watendaji
wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wawakilishi kutoka Korea
Eximbank ya nchini Korea ambapo kazi ya Usanifu mradi huo itapitia hatua
tofauti na kukamilika Novemba 2019.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
mradi huo, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dorothy Mwanyika alisema uzinduzi wa
kazi ya kusanifu uanzishaji miundombinu ya upatikanaji taarifa za ardhi nchini
Tanzania siyo tu utasaidia wananchi katika masuala ya umiliki wa ardhi bali
utawezesha kubuni, kusanifu na kujenga miundombinu kama vile Barabara, Reli,
Majengo pamoja na Miradi mikubwa.
Kwa mujibu wa Mwanyika,
Mradi wa Uanzishaji Miundombinu ya upatikanaji taarifa za ardhi utasaidia pia katika
kukusanya mapato ya serikali kupitia sekta ya ardhi kwa kuwa maeneo ya wamiliki
ya ardhi yatakuwa yameainishwa na hivyo kuwa rahisi wamiliki wake kutambulika
na kusisitiza kuwa Wizara yake itafanya kila jitihada kuhakikisha mradi huo
unakamilika kwa manufaa ya Taifa.
Kwa upande wake Mratibu
wa Mradi huo, Erick Mwaikambo alisema, uzinduzi wa mradi huo utawezesha
upatikanaji ramani za msingi pamoja na taarifa zinazowezesha upimaji ardhi
kufanyika kwa haraka na kwa kasi na kwa bei nafuu na kuwezesha maeneo mengi nchi
kupimwa pamoja na wananchi kupata miliki kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Mwaikambo,
mbali na mambo mengine mradi huo pia utasaidia upatikanaji ramani zitakazotumika
kuandaa matumizi ya ardhi na hivyo kurahisisha kuwepo kwa miji iliyopangwa pamoja
na kuondoa migogoro katika maeneo ya vijijini ikiwemo ile migogoro ya wakulima
na wafugaji.
Mratibu huyo wa Mradi
wa kuanzisha Miundombinu ya Upatikanaji
Taarifa za Ardhi aliongeza kwa kusema kuwa, mradi huo utasaidia pia shughuli za
kubuni, kusanifu na kujenga miundombinu sambamba na kuwezesha kutunza mazingira
na maliasili na Sensa ya watu na makazi na hivyo kusaidia zoezi la kupiga kura
wakati wa uchaguzi.
Mradi wa Kusanifu
Uanzishaji Miundombinu ya Upatikanaji Taarifa za Ardhi nchini Tanzania
unafadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kiuchumi wa nchi
hiyo na Benki ya Exim ya Korea (Korea Eximbank).
No comments:
Post a Comment