HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 14, 2019

Wachimbaji Wasisitizwa Matumizi Salama ya Kemikali

Mwenyekiti wa Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha (aliyesimama), akiongea wakati wa Mkutano wa viongozi wa wachimbaji wa madini ya dhahabu Wilaya ya Chunya na viongozi kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ambao ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi na Mkemia Mkuu wa Serikali (hawapo pichani). 

Na Sylivester Omary

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Esther Hellen Jason amewataka wachimbaji wa madini ya dhahabu wa Chunya kuzingatia matumizi salama ya kemikali wanazozitumia katika shughuli zao za uchimbaji kwa lengo la kulinda afya na mazingira.

Prof. Esther Hellen Jason ameyasema hayo wilayani Chunya wakati akiongea na viongozi wa wachimbaji na wamiliki wa migodi ya madini ya dhahabu.

"Ndugu zangu tuzingatie matumizi salama ya kemikali kwa lengo la kulinda mazingira, afya zetu na vizazi vyetu, tunatambua sekta ya madini ni moja ya sekta muhimu sana katika kukuza uchumi wa nchi kwa sababu dhahabu inaingiza mapato ndani ya Serikali lakini huwezi kuipata dhahabu bila kutumia baadhi ya kemikali." Alisema Prof. Jason.

Ameongeza kuwa, kukutana na wadau na kujadiliana namna bora ya kuimarisha mahusiano ya kikazi ni njia sahihi ya kutatua changamoto na kuboresha utendaji kazi wa pande zote katika shughuli hizi za uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu.

Hivyo changamoto zenu mlizowasilisha leo tunazichukua kwa uzito mkubwa na tutayafanyia kazi ili kuboresha zaidi utendaji wetu na shughuli zenu.

“Kwa zile zilizo ndani ya uwezo wa Bodi ya Wakurugenzi tutazifanyia kazi kwa lengo la kurahisisha utendaji wenu na zinayohitaji maamuzi ya juu zaidi tutayawasilisha ili kupatiwa ufumbuzi maana zikitatuliwa changamoto hizi tunaamini hazitakuwa kwa faida ya Chunya tu bali kwa wachimbaji wa Tanzania nzima wanaotumia kemikali." Alimalizia

Kwa upande wake, Mkemia Mkuu wa Serikali, Dkt. Fidelice Mafumiko, alisema mkutano huo ni mwanzo wa ushirikiano wa Mamlaka na wachimbaji hao wenye lengo la kutatua changamoto na kuzifanya kuwa fursa za kuboresha utendaji na kuwezesha wadau hao wa Chunya na maeneo mengine ya migodi nchini.

Akiongea kwa niaba ya wachimbaji, Mwenyekiti wa Wachimbaji wa dhahabu Mkoa wa Mbeya, Leonard Manyesha, alisema anashukuru kwa mkutano huo na anaamini mazuri yaliyojadiliwa yataleta tija yakifanyiwa kazi.

"Nimefurahishwa na mkutano huu na naamini tuliyojadili yakifanyiwa kazi yataleta tija kwenye kazi zetu za uchimbaji wa dhahabu. Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali wamekuwa karibu sana kwetu hasa kwenye mafunzo ya matumizi salama ya kemikali na kutatua changamoto zetu pale tunapoziwasilisha." Alisema Manyesha.

No comments:

Post a Comment

Pages