Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, akitoka katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya kesi yake kushindwa kusikilizwa leo.
Janeth Jovin
Janeth Jovin
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea kusikiliza ushahidi wa kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kutokana na upande wa mashitaka kukosa kibali cha kuita mashahidi kutoka mkoani Kigoma.
Hayo yamebainishwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja mahakamani hapo kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa.
Katika kesi hiyo ambayo ilipaswa kuendelea kwa shahidi wa tano, Wakili Katuga amedai kuwa shauri hilo lilipangwa kusikilizwa na walishaanza utaratibu wa kupata mashahidi kutokea mkoani Kigoma lakini wamekosa kibali kutoka kwa Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu.
Wakili Katuga ameiomba mahakama ifanye ahirisho wakati wakifatilia kibali hicho ili wawapate mashahidi hao ambao ni takribani sita kutokea mkoani Kigoma.
Baada ya kueleza hayo Hakimu Shaidi ameahirisha kesi hiyo hadi Juni 16 na 17, 2019.
Katika kesi ya msingi, Zitto anakabiliwa na mashtaka matatu ya uchochezi anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.
No comments:
Post a Comment