HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 27, 2019

RC Kebwe aipongeza Petrobena kwa kusaidia vijana wanaolima mpunga

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Kebwe Steven Kebwa (kulia), akiteta jambo Mkurugenzi Mtendaji Kampuni ya PETROBENA East Africa,Bw.Peter  Kumalilwa alipotembelea kujionea maendeleo ya kilimo cha mpunga la vijana huko Msowela Wilayani Kilosa ambao wamefadhiliwa na kampuni hiyo hivi karibuni.


Na Mwandishi Wetu, Morogoro
 
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dk.Kebwe Steven Kebwe, ameipongeza Kampuni ya Petrobena EastAfrica kwa kufadhili mradi wa kilimo cha mpunga wa eka 50 unaoendeshwa na kikundi cha vijana   cha AgriAjira katika Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro.
 
Akizungumza na waandishi wa habari alipofanya ziara katika shamba la vijana, Dk.Kebwe amesema juhudi za kikundi hicho zitasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kutengeneza ajira nyingi kwa vijana.
 
 “Naipongeza sana Kampuni ya Petrobena kwa kufadhili mradi huu kwa kuwapatia pembejeo za kilimo zikiwemo mbegu,mbolea na elimu bora ya kilimo mambo ambayo kwa pamoja yamewafanya kufikia  hatua  nzuri katika kilimo cha mpunga na kufikia hatua ya kuvuna mpunga safi,” amesema Dk. Kebwe.
 
Amesema mradi wa AgriAjira ni ushahidi tosha kwamba  kuwekeza vizuri katika kilimo kutazaa ajira za uhakika kwa asilimia kubwa ya wananchi Tanzania na ambao ni vijana.
 
“Hatua iliyofikiwa katika shamba hili ni nzuri. Sisi kama serikali nitahakikisha viongozi wa wizara vinazohusika na kilimo, biashara na viwanda wanafika katika eneo hili ili wajionee mradi huu na kuwahakikisha soko la mpunga utakaovunwa,” alisema Dk. Kebwe.
 
Aidha Dk. Kebwe aliwaomba wadau wa maendeleo kujitokeza kuunga mkono miradi mbalimbali inayoanzishwa na vijana hasa katika sekta ya kilimo ili kuwatengenezea ajira vijana kupitia miradi yenye tija kiuchumi na kijamii kwa mendeleo ya taifa.
 
“Serikali ya Awamu ya Tano imejielekeza kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ambao msingi wake mkubwa unategemea sekta ya kilimo ambayo huzalisha malighafi ambazo zitachochea uanzishwaji na uendelezaji wa viwanda na kupelekea uchumi wa nchi kukua,” amesema Dk.Kebwe
Ameleza kuwa  ni lazima kuwekeza katika sekta ya kilimo ambayo ni muhimili mkuu katika ujenzi wa viwanda na biashara kwa ujuml na kuongeza kuwa  nguvu kubwa ielekezwe kwenye kuwajengea uwezo wananchi katika kukifanya kilimo kiwe na tija.
 
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Petrobena East Africa, Bw.Peter Kumalilwa, amesema kampuni yake imejikita katika kushiriki kuendeleza sekta ya kilimo nchini kwa kusambaza mbolea za YARA na pia kutoa elimu na kanuni bora za kilimo ili kukuza uzalishaji mazao nchini.
 
“Tumefadhili mradi huu wa kilimo cha mpunga lengo tu likiwa ni kutengezea ajira kwa vijana na pia kukuza uzalishaji wa mazao ili azma ya serikali ya awamu ya tano kufikia uchumi wa kati na viwanda ifikapo 2025 ifikiwe,” amesema Bw. Kumalilwa.
 
 Mwakilishi wa  AgriAjira,  Bw January Njavike, amemuomba   Mkuu wa Mkoa kuwaunganisha na masoko ili mazao yao yapate soko.
 
“Tunaishukuru Serikali ya Mkoa huu kwa kutupatia ardhi,Kampuni  ya Petrobena kwa kutufadhili  pia Wakala wa Mbegu (ASA) na kampuni ya Mbolea ya YARA Tanzania kwa kuendelea kutupa ushirikianao katika kufanya kilimo cha kisasa,” alisema Bw. Njavike

No comments:

Post a Comment

Pages