HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

June 25, 2019

Shell Tanzania yahamasisha nishati mbadala

Mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo ya uongozi na ujasiriamali Dk. Donath Olomi (kulia), akiwa kwenye picha ya pamoja na washindi wa shindano ya  nishati mbadala.  Kabla ya kuanza  kwa meza ya majadiliano kati ya  kampuni ya Shell Tanzania nawadau wake  kutoka  Sekta mbalimbali ikiwemo  nishati mbadala  na mazingira iliyofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. Kushoto ni mshindi wa kwanza Bw. Leonard Kushoka wapili kushoto ni  Anyelwisye Mahenge (mshindi wa tatu) na wapili kulia ni  philip Mtui (mshindi wa pili).


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
 
WADAU mbalimbali wa mazingira wamepongeza juhudi zinazofanywa na Kampuni ya Shell Tanzania na hasa katika kuchangia eneo la utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza athari za nchi kugeuka jangwa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya kumalizika kwa mjadala ulioandaliwa na kampuni hiyo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yanayosababishwa na uharibifu mkubwa wa mazingira, wadau wengi hawakusita kuipongeza Shell Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele kuhimiza matumizi bora ya nishati mbadala ili kulinda mazingira.

Mwakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Bw. Joseph Qamara, alisema serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika suala zima la uhifadhi na utunzaji wa mazingira ili kuliepusha taifa majanga mbalimbali yatokanayo na mabadiliko ya tabia nchi.

“Tunatambua juhudi na vipaumbele vya Shell Tanzania na wadau wengine katika kuhamasisha utunzaji wa mazingira kwa kuepuka uharibifu wa misitu, na badala yake kuhamasiaha matumizi ya nishati mbadala pamoja na upandaji wa miti,” Bw. Qamara alisema.

Majadiliano hayo yaliwashirikisha washindi wa shindano maalum la mashujaa wazalishaji wa nishati mbadala ya mkaa, lililozinduliwa rasmi mwaka jana na ofisi wa makamu wa raisi - idara ya mazingira, ambao ubunifu wao unalenga kuongeza uzalishaji wa mkaa mbadala utakao saidia kuokoa misitu na kuboresha mazingira kwa ujumla,waliishukuru kampuni hiyo kwa kuwawezesha.

Kampuni ya Shell Tanzania ilitoa shilingi milioni 300 kwa mshindi wa kwanza, shilingi 200 kwa mshindi wa pili na shilingi milioni 100 kwa mshindi wa tatu kama mtaji ambao utawekezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kama sehemu ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala.

Mkurugenzi wa taasisi ya uongozi na biashara (IMED) Dkt. Donath Olomi, mbali ya kuipongeza Kampuni ya Shell Tanzania alisema mjadala ulikuwa na faida kubwa kwani uliwaleta pamoja wadau wote muhimu kwenye maeneo ambayo yalikuwa yakijadiliwa kwa uwazi mkubwa.

Dkt. Olomi alisema kuwa ushiriki wa serikali ni muhimu katika kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati mbadala badala ya mkaa na kuni, hatua ambayo itasaidia kupunguza uharibifu wa mazingira unaochangiwa zaidi na ukataji wa kuni na utengenezaji wa mkaa unaotumiwa kama chanzo kikuu cha nishati majumbani.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ShellTanzania Bwana Marc den Hartog, alisema kuwa ipo haja ya watanzania kubadilika kutoka katika matumizi ya mkaa na kuni na kuelekea kwenye matumizi ya nishati mbadala, hatua ambayo itaepusha athari zote zinazoletwa na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na ukame.

“Sisi Shell Tanzania tutaendelea kuwa mstari wa mbele kushirikiana na serikali na wadau wengine kuhamasisha utunzaji wa mazingira na kuepuka namna yoyote inayoweza kuchochea mabadiliko ya tabia nchi yatakayoleta athari nchini,” alisema der Hartog ambaye kampuni yake inashiriki katika harakati za uchimbaji gesi asilia iliyosindikwa nchini Tanzania.

Alisisitiza kuwa mabadiliko ya tabia nchi hayana budi kupewa umuhimu mkubwa, na kuhakikisha kuwa wadau wote muhimu wanaunganisha nguvu katika kuhakikisha hayaleti athari hasi kwa taifa na maisha ya wananchi kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages