Mwenyekiti wa Baraza la
wafanyakazi wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambaye pia ni Kaimu Mtendaji
Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, akisoma taarifa ya utekelezaji wa Wakala huo
kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi),
Arch. Elius Mwakalinga, katika kikao cha Baraza la wafanyakazi jijini Dodoma,
leo.
Katibu Mkuu wa Wizara
ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Arch. Elius Mwakalinga,
akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Baraza la wafanyakazi wa Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), jijini Dodoma. PICHA
NA WUUM.
Dodoma, Tanzania
Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), umetakiwa kutekeleza miradi
wanayoisimamia kwa wakati na kuzingatia weledi ili kuongeza tija na uzalishaji
katika Wakala huo.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Arch. Elius Mwakalinga, wakati akifungua kikao
cha siku mbili cha Baraza la wafanyakazi wa Wakala huo, jijini Dodoma.
Agizo la Katibu Mkuu huyo limefuatia baada ya kupata malalamiko kutoka kwa
baadhi ya wateja wa Wakala huo amabapo wamesema kuwa Wakala huo umekuwa ukichelewesha
miradi, hivyo amewataka kupitia Baraza hilo kujiwekea malengo na mpango mkakati
wa kutekeleza miradi hiyo na kuikamilisha kwa wakati.
“Nina uhakiaka suala hili lipo chini ya uwezo wenu endapo mtajipanga
vizuri na kufanya kazi kwa mshikamano na weledi huku mkithamini mchango wa kila
mmoja wenu katika eneo la kazi, basi mtafanikiwa,” amesema Mwakalinga.
Aidha, ameutaka Wakala huo kujiwekea maazimio yatakayowasilishwa
Wizarani ambayo yatajikita katika uboreshaji wa maslahi ya watumishi,
ikiwemo kuwajengea uwezo utakaowafanya
kutimiza majukumu yao kwa wakati na ufanisi zaidi.
Kuhusu madai ambayo Wakala unadai Taasisi nyingine za umma, Katibu Mkuu
Mwakalinga ameutoa hofu Wakala huo kwa kusema kuwa suala hilo halitafumbiwa
macho na atahakikisha kuwa madeni yote yanalipwa baada ya kuhakikiwa.
“Wekeni kumbukumbu zenu za madai vizuri ili ziweze kuhakikiwa kabla ya
kuwasilishwa kwa wahusika, nami naahidi kufuatilia madeni haya na kuhakikisha
kuwa yatalipwa,” amesisitiza Katibu Mkuu.
Ameongeza kuwa Serikali inathamini mchango wa Wakala huo katika kufikia
uchumi wa kati kupitia viwanda ambapo amefafanua kuwa Wizara yake pamoja na
Taasisi zilizo chini yake imejiwekea agenda madhubuti ambazo anaamini zikitekelezwa
basi Sekta ya Ujenzi nchini itakuwa kwa kasi.
Naye, Kaimu Mtendaji Mkuu wa TBA Arch. Daudi Kondoro amemhakikishia Katibu
Mkuu huyo kuwa atatekeleza maagizo yote na pia atahakikisha maazimio watakayo
jiwekea yanatekelezwa kwa wakati.
Alisema kuwa taratibu za kupandisha watumishi vyeo zinaendelea ambapo
tayari watumishi 64 waliokidhi vigezo wamepandishwa vyeo katika madaraja
mbalimbali na watumishi 17 wamebadilishwa kada kulingana na taaluma zao.
Kikao hicho kimejumuisha zaidi ya wajumbe 62 ambao baadhi yao ni wakuu
wa idara na vitengo, mameneja kutoka mikoa yote, wawakilishi wa wafanya kazi
kutoka idara na vitengo pamoja na wawakilishi kutoka vyama vya wafanyakazi
vilivyomo ndani ya Wakala.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment