Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira
na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama (kushoto) pamoja na Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke (katikati)
wakimkabidhi Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye
Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa (kulia) Kiti Mwendo “Wheelchair” ikiwa ni sehemu ya
maabidhiano wakati wa hafla hiyo.
Balozi wa China Nchini Tanzania Bi. Wang Ke akimkabidhi cherehani
kwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma, Mhe. Fatma Toufiq wakati wa hafla
hiyo iliyofanyika Jijini Dodoma.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama amepokea cherehani na vifaa siadizi kwa ajili ya Watu
wenye Ulemavu vilivyotolewa na Ubalozi wa China nchini.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo fupi ya makabidhiano iliyofanyika katika ofisi ndogo za ubalozi huo zilizopo
Jijini Dodoma, Waziri Mhagama alieleza kuwa Serikali inatambua haki za Watu
wenye Ulemavu nchini hivyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa
maendeleo ili kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki zao stahiki ikiwemo kuwapatia vifaa saidizi.
“Vifaa saidizi ni muhimu kwa
kundi hilo maalumu kwa kuwa vinawawezesha kumudu mazingira yanayowazunguka na
kuwasaidia kufanya shughuli zao za kila siku bila kukabiliana na changamoto,” alisema Mhe. Mhagama
Alieleza kuwa kutokana na vifaa
hivyo kuwa ni ghali na upatikanaji wake umekuwa mgumu na kupelekea watu wenye
ulemavu kushindwa kuvinunua, Serikali imeendelea kutenga bajeti kwa ajili ya
kununua vifaa hivyo.
Aliongeza kuwa, katika ujenzi
wa uchumi wa viwanda Serikali kupitia Shirika la kuhudumia viwanda Vidogovidogo (SIDO) kushirikiana
na wadau imejipanga kuimarisha utengeneza wa baadhi ya vifaa hivyo,
vitakavyokuwa vinapatikana hapa nchini.
Aidha alitoa wito kwa jamii kubadili
mtazamo na fikra potofu juu ya watu wenye ulemavu, bali watambue kundi hilo
linaweza na linamchango mkubwa katika jamii na nchi kwa ujumla.
Kwa upande wake, Balozi wa
China nchini Tanzania, Bi. Wang Ke alisema kuwa Serikali ya China itaendelea
kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali
pamoja na kuendelea kutoa misaada kwa ajili ya wenye uhitaji.
Naye Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa aliwataka wadau
ndani na nje ya nchi kuendelea kujitokeza na kusaidia makundi yenye uhitaji
maalumu, kwa kuunga mkono juhudi za Serikali katika kusaidia masuala ya Watu
wenye Ulemavu.
Katika hafla hiyo pia aliudhuria
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala
ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dodoma,
Mhe. Fatma Toufiq na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mwanza Mhe. Kemilembe Lwota.
No comments:
Post a Comment