HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 02, 2019

FC VITO SINGIDA YAAGWA, TFF YAZIPONGEZA TAASISI ZA SDA NA LIIKE FINLAND

 Balozi wa Finland nchini Tanzania, Riitta Swan, akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga wachezaji wa FC Vito Singida walioondoka nchini alfajiri ya leo.
 Kocha wa FC Vito Singida, Mohamed Kweka, akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuwaaga FC Vito Singida, walioondoka kwenda Finland kushiriki Helsinki Cup 2019.
 Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo mwenye tshirt nyeupe akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Filand kulia kwake na wachezaji wa FC Vito.
 Mratibu wa SDA, Ramson Lucas, akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuwaaga FC Vito Singida, walioondoka kwenda Finlnda kushiriki Helsinki Cup 2019.
Mwakilishi wa LiiKe Finland, Anu Nieminen, akizungumza na wageni waalikwa wakati wa hafla ya kuwaaga FC Vito Singida, walioondoka kwenda Finland kushiriki Helsinki Cup 2019.
 Mwakilishi wa TTU Singida, Arnold Bugado akizungumza wakati wa kuiaga FC Vito Singida jijini Dar es Salaam.


NA SALUM MKANDEMBA, DAR ES SALAAM

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limezipongeza Taasisi za Sports Development Aid (SDA) ya Tanzania na LiiKe Finland ya nchini Finland, kwa aina ya uwekezaji wanaofanya katika kuratibu na kuendesha timu wanazomiliki kwa ubia za FC Vito za hapa nchini. 

Pongezi hizo zimetolewa Jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Oscar Mirambo, wakati akikabidhi bendera ya Taifa kwa kikosi cha FC Vito Singida, ya mjini Singida, iliyoondoka leo kwenda Helsinki, kushiriki michuano ya Helsinki Cup 2019.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga FC Vito Singida, Mirambo alisema jitihada zinazofanywa na SDA na LiiKe Finland, zinaunga mkono jitihada za Serikali na TFF katika kufanya uwekezaji kwenye soka la vijana, na kuwataka kuongeza jitihada katika kuwafikia vijana na watoto wengi zaidi nchini.

Mirambo, ambaye ameiongoza timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ kama Kocha Mkuu mwenye mafanikio zaidi, aliwataka nyota 12 wanaounda FC Vito Singida kuitumia vema fursa waliyopata kwa kupigania vema bendera ya taifa na kurejea na ushindi.

FC Vito Singida, inayomilikiwa kwa ubia kati ya SDA na LiiKe Finland, inaenda Finland kushiriki michuano ya Helsinki Cup 2019, ambako waliagwa jana katika ofisi za Ubalozi wa Finland jijini Dar es Salaam, ambako Mirambo alimuwakilisha Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao aliyepaswa kuwa mgeni rasmi.

Katika hafla ya kuwaaga, Mirambo aliwapongeza SDA na LiiKe, kufanikisha ushiriki wa FC Vito Singida katika michuano ya Helsinki Cup, michuano ya nne kwa ukubwa barani Ulaya, miongoni mwa mashindano ya vijana, yanayokusanya pamoja zaidi ya vijana 1,300 kutoka mataifa zaidi ya 20 duniani.

Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha vijana chini ya miaka 12 ni Fred Petro, Jovine Kabeya, Philipo Mwigema, Samson Jackson, Simon Bugado, Raphael Raphael, Asajile Lisu, Hudhaifa Kweka, Omari Ismail, Elia Makhata, Kelvin Tikae na Maregesi Dominick, wakiwa chini ya kocha wao Mohamed Kweka.

Alisema jambo lilofanywa na SDA na LiiKe pamoja na ubalozi wa Finland ni somo kwa kwa wadau wengine kujifunza na kuona ni kwa namna gani wanaweza kutoa mchango wao kuwasaidia vijana wa Kitanzania kuonesha uwezo wao ili mataifa mengine yajue kama kuna vipaji.

“Niwapongeze wote mliofanikisha kuandaa safari hii, lakini pia niwaombe vijana mnaenda kutuwakilisha kuhakikisha mnaenda kupeperusha vyema bendera kwa kurudi na kombe , lakini mkumbuke kuishi kwenye maadili ya tabia njema kwa sababu mnaenda kukutana na vijana kutoka mataifa mbalimbali,” alisema Mirambo.

Kwa upande wake Balozi wa Finland nchini, Riitta Swan, alisema michezo humsaidia mwanafunzi kujijenga kiakili kwa kuwa tayari kujifunza mambo mabilimbali, huku akienda mbali zaidi kwa kuahidi kuendelea kusapoti jitihada za SDA na LiiKe Finland katika kufanikisha safari za mwaka za FC Vito.

“Hivyo nawatakia safari njema vijana wa FC Vito Singida kwenda kuiwakilisha nchi yenu kwa kufanya vizuri, lakini mkajitume kwa kuwa michezo kwa sasa ni ajira kubwa dunia, tutaendelea kufanya kazi kwa kushirikiana na Serikaliya Tanzania kuendelea kupeleka vijana kila mwaka,” alisema Swan.

Naye Mratibu wa SDA, Ramson Lucas, aalisema taasisi yake inajivunia uwezeshaji kielimu na kimichezo inaoutoa kwa vijana wanaoenda Finland kila mwaka, ambako licha ya kujifunza na kutaua weledi katika soka, pia hupata familia rafiki wanaowasaidia katika masomo yao.

“Ukiondoa nafasi ya kujifunza soka kupitia Helsinki Cup, vijana wanaokwenda Finland kila mwaka, utaratibu ulioanza mapema miaka ya 2000, wameweza kupata familia rafiki kule, zinazowasaidia katika masomo yao ya elimu ya msingi hadi sekondari,” alisema Ramson.

No comments:

Post a Comment

Pages