Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw.Japhet Justine (kulia) akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa kiwanda cha kahawa cha TANICA. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti muda mfupi baada ya kutembelea kiwanda hicho mjini Bukoba hivi karibuni. TADB imeahidi kukiongezea nguvu kiwanda hicho ili kiongeze uzalisahaji zaidi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Bw.Japhet Justine (kulia) akijadiliana jambo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti muda mfupi kabla ya kutembelea kiwanda cha kahawa cha TANICA mjini Bukoba hivi karibuni.TADB imeahidi kukiongezea nguvu kiwanda hicho ili kiongeze uzalisahaji zaidi.
Na Mwandishi Wetu, Kagera
BENKI ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) imeahidi kukiongezea uwezo kiwanda cha Tanganyika Instant Coffee (TANICA) kinachochakata kahawa mkoani Kagera kwa lengo la kukuza mnyororo wa thamani wa zao
hilo nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara yake mkoani humu, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Bw.Japhet Justine amesema ni muhimu kuongeza nguvu kiwanda hiki kwani kuwepo kwake kunaatoa soko la uhakika kwa wakulima wa kahawa.
‘’TADB imedhamiria kukiendeleza kiwanda cha TANICA ili kuchakate kahawa hapa hapa na kuiongezea thamani na kuifanya iwe ni kahawa yenye ushindani katika soko la ndani na nje,” amesema Bw.Justine.
Amesema kuna kila sababu ya kukiongezea nguvu kiwanda hicho kwani kuchakata kahawa kutachangia kutengeneza ajira, pia kutasaidia kujenga soko la ndani la uhakika la kahawa kwa wakulima na kuchochea uzalishaji na ubora wa kahawa.
“ Benki ilitoa mkopo wa shilingi bilioni 30 katika msimu wa mwaka jana zitumike katika zoezi la ukusanyaji na ununuzi wa kahawa kutoka kwa wakulima mkoani humu. Kwa mafanikio yaliyopatikana katika zao la msimu uliopita, tunataka msimu huu mgao wa kwanza uende TANICA ili
kahawa yetu ichakatwe hapa hapa nchini ili thamani yake iongezeke,’’ ameeleza Bw.Justine.
Amekumbusha kwamba kiwanda kama hicho kipo toka 1963, na kuongeza kwamba kikiendelezwa kahawa ya Tanzania itapanda thamani itawavutia wanunuzi wa ndani na nje, na kuwafanya Watanzania kutumia kahawa iliyotengeneza hapa hapa nchini.
Amesema kwa sababu ya juhudi ya pamoja ya msimu uliopita kahawa imezalishwa kwa wingi na imekuwa na ubora unaotakiwa katika soko na kusema ni muhimu sasa kujikita katika kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata kahawa ili kuiongezea thamani na kuifanya kahawa ya Tanzania kuwa ya ushindani katika masoko ya nje.
‘’Tunaendelea kutekeleza kwa vitendo azma ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk.John Magufuli ya kujenga uchumi wa kati na wa viwanda ifikapo mwaka 2025. Na hili limejidhihirisha kupitia mafanikio yanayoonekana kwa wakulima,’’ amesema Bw. Justine.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, ameishukuru Benki ya TADB kwa ushirikiano ambao amesema umeleta mafanikio katika kuboresha na kukuza uzalishaji wa zao la kahawa mkoani Kagera. ‘’Mkoa utaendelea kutoa ushirikiano katika uamuzi wa TADB wa
kukiendeleza kiwanda cha TANICA jambo hili litachochea ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa vijana,’’ alisema Bw. Gaguti.
Amesema azma ya serikali ni kujenga viwanda nchini, hivyo kwa kukiendeleza kiwanda cha TANICA kunaonyesha agizo la serikali kujenga viwanda umefanyiwa kazi na watendaji wake.
No comments:
Post a Comment