Regina Msoka akieleza jinsi vipande vya korosho vinavyowezwa kubadilishwa kuwa siagi.
IMEELEZWA kuwa utumiaji wa vipande vya korosho vinavyobaki katika korosho zilizobanguliwa zinaweza kubadilishwa matumizi na kutengenezewa siagi.
Akizungumza katika maonesho ya 43 ya Kimataifa ya Biashara katika banda la Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) Mtafiti kutoka kituo cha utafiti wa kilimo Nalindili Mtwara, Regina Msoka anasema wakulima wameanza kubuni njia hiyo ili kuweza kuliongezea thamani zao hilo la korosho.
Anasema katika ubanguaji wa korosho kuna hatua za upandaji wa daraja ambazo zile zinazobanguliwa zikiwa nzima na kubwa bei yake inakuwa juu lakini vipande vinavyovunjika uwa na bei ndogo.
"Katika kupanda madaraja hayo vile vipande vinavyovunjika bei yake inakuwa chini hivyo korosho hizo ndizo zinachukuliwa na kuongezewa thamani kwa kutengeneza siagi za korosho.
Kwa sasa wakulima wameshaanza kugundua njia hii ambayo licha ya kuliongezea zao hilo thamani lakini pia uwapatia fedha ambazo zinawawezesha kujikwamua na chamgamoto mbalimbali za maisha, " anasema.
Anasema kwa kilo moja ya vipande vya korosho wanaweza kupata chupa nne za siagi zenye thamani ya Sh. 20,000, wakati vipande hivyo uuzwa kwa kilo Sh. 10,000.
Aidha anasema bidhaa zingine wanazotengeneza kutokana na vipande vya korosho ni maziwa ya korosho.
"Kwa kilo moja ya vipande vya korosho vinavyotengeneza maziwa tunapata kiasi cha Sh. 20,000 hadi 25,000, mimi nawaomba wakulima wahakikishe wanalitumia zao hili vizuri, " anasema.
Aidha Msoka amewataka wakulima wakorosha kuendelea kulima zao hilo kwani linafaida nyingi lakini pia amewaomba watanzania kula korosho kwa wingi kwani ni nzuri kwa afya.
"Watanzania wenzangu tuleni korosho ili tuendelee kuwapa nguvu wakulima wetu kulima zao hili, na sisi wabunifu tutaendelea kubunifu vitu mbalimbali vinavyotokana na korosho, " anasema.
No comments:
Post a Comment