HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 03, 2019

Mkuchika: Nchi inahitaji uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya haraka

Na Janeth Jovin

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala bora, Kapten Mstaafu George Mkuchika amesema kuwa Tanzania inahitaji uchumi wa viwanda ili kuleta mageuzi ya haraka na kuimarisha uchumi wa nchi.

Hata hivyo Waziri Mkuchika amesema malengo hayo yanaweza yasifanikiwe kama vitendo vya rushwa nchini vitaendelea na kushindwa kudhibitiwa.

Waziri Mkuchika ameyasema hayo leo katika Kongamano la siku maalum ya kutafakari masuala ya Rushwa katika maonesho ya 43 ya kimataifa ya biashara yanayofanyika kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

Anasema nchi yoyote ili iweze kupambana na vitendo vya rushwa ni lazima kuwepo na utashi wa kisiasa ambao unaweze kupatikana  kwa viongozi wa juu.

"Katika kipindi hiki cha Serikali ya awamu ya tano tumefanikiwa kupunguza vitendo vya rushwa nchini,  moja ya mafanikio ya wazi yaliyopatikana kutokana na kudhibiti mianya ya rushwa ni kuimarika kwa uwajibikaji,  upatikanaji wa elimu bore pamoja na ongezeko la mapato, " anasema.

Anasema hayo mafanikio yanatokana na usimamizi imara wa mapambano dhidi ya rushwa yanayoongozwa na Rais John Magufuli.

Hata hivyo Mkuchika anasema mapambano dhidi ya rushwa nchini yanakwamishwa na viongozi ambao sio waadilifu hivyo ni muhimu wakabadilika.

Aidha alisema kwa kutambua umuhimu wa sekta ya viwanda na biashara katika kukuza uchumi, serikali imefanya jitihada ya kukaa na wafanyabiashara na kusikiliza kero zao kwa lengo la kuzitatua kwa haraka.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade),  Edwin Rutageruka anasema wanaipongeza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa kazi kubwa wanayoifanya juu ya mapambano dhidi ya rushwa.

No comments:

Post a Comment

Pages