HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 03, 2019

Shirika la Posta lafurahia ongezeko la utumaji wa barua nchini

Meneja wa Barua na Usafirishaji wa Shirika la Posta Hadija Iddi akizungumza na Waandishi wa habari (hawapo pichani).
 
Na Janeth  Jovin

SHIRIKA la Posta Tanzania limesema kuwa ongezeko la  utumaji barua limeongezeka kutoka asilimia 26 ya mwaka 2016/17 hadi kufikia asilimia 36 kwa mwaka 2018/19.

Akizungumza ndani ya banda la maonyesho ya Shirika hilo lililopo kwenye viwanja vya maonyesho ya 43 ya biashara ya kimataifa Kaimu Meneja wa barua na usafirishaji wa Shirika hilo,  Hadija Iddi anasema ongezeko hilo ni la  barua za ndani ambazo ni za kuomba kazi, nyaraka za mashuleni na  za maofisini.

Anasema barua za nje kwa mwaka 2016/17 zilishuka kwa asilimia 50, lakini mwaka 2017/18/ zikapanda kwa asilimia 37.

Aidha Iddi anasema baada ya kuanzishwa kwa huduma ya stempu mtandao mwaka 2016 ongezeko la mauzo a stempu hizo mwaka 2017/18 yalipanda kwa asilimia 36 ukilinganisha na kiwango kidogo kilichouzwa mwaka 2016 wakati ilipoanzishwa.

Anasema matumizi ya mtandao, hayajaathiri utumaji barua, kutokana na kuwepo kwa nyaraka ambazo zinahitaji kutumwa kwa njia ya Posta na Shirika lao linaaminika hivyo wateja wao bado wanatumia.

kwa upande wa mauzo ya  stempu za kumbukumbu kwa ajili ya vivutio vya utalii, wanyama, picha za watu mashuhuri, Iddi anasema mauzo hayo yalipanda kwa asilimia saba mwaka  2017/18.

Anasema biashara hizo za stempu za kumbukumbu zimekuwa zikifanywa zaidi na nchi za nje zikiwamo China, Marekani, Canada, Uingereza, Indonesia, Italia, India na Autralia.

Anasema biashara hiyo ya stempu za kumbukumbu imekuwa kwa sababu ya kuanzisha kwa huduma ya stempu mtandao.

"Huduma hiyo mtu anaomba mtandaoni, nalipia mtandaoni halafu tunamsafirishia popote alipo" alisema Iddi.

Iddi alifafanua kuwa mbali na huduma hizo pia wanatoa huduma ya kusafirisha mizigo ikiwamo  kuhamisha vifaa vya ofisini na majumbani  kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine.

No comments:

Post a Comment

Pages