HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 03, 2019

Serikali yashauriwa kupitia upya Sheria ya wakimbizi

 Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Kitivo cha Sheria, Profesa Khoti Kamanga akitoa mada kwa wadau kuhusu wakimbizi.


Na Suleiman Msuya
 
SERIKALI imeshauriwa kupitia upya Sheria ya Wakimbizi ya mwaka 1998, Sera 2003 na Kanuni zake ili ziweze kuona na mikataba mbalimbali ya kimataifa kuhusu wakimbizi ambayo nchi imeingia.

Ushauri huo umetolewa na Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Sheria Profesa Khoti Khamanga wakati wa semina kwa wadau wa sekta binafsi na Serikali iliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Prof.Kamanga ambaye aliwasilisha mada kuhusu hali ya wakimbizi na umuhimu wa kuwa na nyaraka kwa kundi hilo alisema Sheria ya 1998 na Sera 2003 hazina oani jambo ambalo linaenda kinyume na mikataba mbalimbali ambayo nchi imesaini.

Alisema Tanzania imesaini mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Wawakimbizi wa mwaka 1951, Mkataba wa Umoja wa Afrika 1969 na Mkataba wa Maziwa Makuu 2006 ambayo maelekezo yake hayawezi kutekelezwa kwa Sheria na Sera iliyopo.

"Sheria yetu ni mwaka 1998 Sera ya 2003 lakini kiutaratibu huwa inaanza Sera ndio sheria jambo ambalo halipo. Lakini pia ndani ya Sheria na Sera inahitajika kuona mikataba ya kimataifa ikiwa ndani jambo ambalo halipo," alisema

Alisema katika eneo hilo la wakimbizi ipo mchangamoto za kikahuni hivyo Serikaki inatakiwa kuangalia kwa jicho pana.

Mhadhiri huyo alisema ushauri mwingine ambayo anautoa kwa Serikaki ni kuwarasimisha wakimbizi ili wawe na faida kwa nchi kwa kuongeza mapato kwa kulipa kodi.

Alisema bila sheria kuona na mikataba mbalimbali ambayo nchi imeingia inayopata hasara ni Serikali.

Aidha, alisema idadi ya wakimbizi wanaokimbilia nchi za nchi imepungua ambapo kwa sasa wapo milioni 25 huku wakimbizi zaidi ya milioni 40 wakiwa wanakimbia ndani ya nchi husika.

Prof.Kamanga alisema taarifa zinazooneshwa kuwa wakimbizi kutoka nchi za Afrika kuingia Ulaya sio za kweli kwani idadi kubwa wanakimbilia nchi za Afrika.

"Inakadiriwa kwa sasa wakimbizi wa nje wamepungua ila wa ndani ya nchi wameongezeka. Lakini pia kwa miaka ya sasa Serikaki hazitaki kujali wakimbizi kama zamani," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Wizara ya Mambo ya Ndani anayeshughulikia Makambi na Makazi ya Wakimbizi Nsato Marijani alisema semina hiyo iliyoandaliwa na Taasisi ya Dignity Kwanza imekuja wakati muafaka kwao ili kupata uelewa kuhusu uwepo wa nyaraka sahihi kwa kundi hilo.

Alisema iwapo idadi ya wakimbizi itafahamika itarahisisha Serikali kujipanga na kuwahudumia bila kubahatisha.

Kamishna Marijani alisema kwa mujibu wa takwimu zilizopo Tanzania ina wakimbizi zaidi ya 300,000 huku kila wiki wakirejesha wakimbizi zaidi ya 2,000 makwao kwa hiari.

"Serikali inahitaji ushirikiano na wadau mbalimbali katika kukabiliana na wakimbizi hivyo niwapongeze Dignity Kwanza kwa uamuzi wao wakukutanisha kujadili njia sahihi ya kuwepo kwa nyaraka kwa kundi hilo," alisema.

Akizungumzia semina hiyo Mwasheria wa Dignity Kwanza, Jovin Sanga alisema wamekutanisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi na Serikali kujadiliana namna sahihi ya kuwahudumia wakimbizi na waomba hifadhi.

Alisema semina hiyo itaweka mipango na namna ya kukabiliana na changamoto zinazowakumba wakimbizi na waomba hifadhi.

Sanga alisema wakimbizi wanakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo kutotambuliwa kwa taaluma na vipaji vyao hivyo semina hiyo inaweza kuwa chachu ya kujua njia za kukabiliana nazo.

"Tumeamua kukutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Serikaki sababu kubwa ni kuangalia namna ya kuwafanya wakimbizi wajione ni watu kama wazawa kwa kuonesha vipawa vyao na ujuzi," alisema.

Mwanasheria huyo alisema wapo watu wengi wanaingia nchini katika mazingira ambayo sio ya kikimbizi hivyo wanahitajika kujulikana walipo ili waweze kupata msaada stahiki.

No comments:

Post a Comment

Pages