Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) iliyokutana kwa siku mbili Juni 22 na Juni 23,2019
ilisikiliza mashauri 4 na baadaye kuyatolea hukumu.
Shauri la Kwanza
ERICK AMBAKISYE
Mlalamikiwa
katika shauri hili hakuwepo katika kikao hiki licha ya kwamba taarifa
ya wito ilitumwa kwa njia ya E-mail mnamo tarehe 16 Juni 2019 na kwa EMS
Mnamo tarehe 17 Juni 2019 na risiti ya malipo ya kutumia nyaraka hizo
iliwasilishwa mbele ya kikao kwa ajili ya uthibitisho lakini hata hivyo
Mlalamikiwa hakutokea katika kikao hiki.
Baada ya uthibitisho huo Kikao
kiliazimia kuendelea bila uwepo wa Mlalamikiwa kwakuwa inaonekana
alipata wito lakini hakutoa taarifa yoyote ya udhuru.
Tuhuma
zilizomkabili ERICK AMBAKISYE ni mbili akiwa ni Mwenyekiti wa Chama cha
Mpira wa Miguu Mkoa wa Songwe kama ambavyo zinaonekana katika hati ya
mashtaka.
Pamoja na
tuhuma hizo Mlalamikaji alikuwa na shahidi mmoja Nugu JAMES MHAGAMA
ambaye aliitwa kwa nia ya kuthibitisha tuhuma hizo, ambapo Shahidi
alieleza namna ambavyo Mlalamikiwa alifanya vitendo kinyume na Katiba ya
TFF ikiwemo kutokutoa ushirikiano kwake akiwa kama Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Mashindano ya TFF, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF na
Msimamizi wa RCL Kituo cha Songwe.
Changamoto
kubwa ilikuwa ni kuzuia kwa Maafisa, Waamuzi na watahmini wa mechi
kutokana na deni la Tshs 5,700,000 na hatimaye shahidi huyu kufunguliwa
kesi katika Mahakama ya Mwanzo Mkoani Songwe na kuwekwa ndani kwa siku
tatu baada ya kukosa dhamana kitendo kilichofanywa na mmiliki wa hoteli
ya Mkulima ambayo viongozi waliyofikia.
Pamoja
na juhudi zote za kusuluhisha mgogoro huu na fedha kulipwa lakini
Mmiliki wa hotel aliendelea kuwaghasi viongozi hao kwa kushirikiana na
Mlalamikiwa. Kimsingi Mwenyekiti alitoa taarifa kuwa maandalizi
yamekamilika na kila kitu kinaenda sawa jambo ambalo si kweli na
hakuwahi kuonekana kipindi chote cha mashindano kuanzia tarehe 27 Machi
2019 hadi 9 Aprili 2019. Shahidi alifafanua zaidi kwa kusema kwamba
mwenye mamlaka ya kuomba kituo ni Mkoa husika baada ya kujiridhisha kuwa
umekamilisha maandalizi yote kwa ajili ya kuendesha mashindano ya RCL.
Wajumbe
walipata fursa ya kumuuliza shahidi maswali mbali mbali kuhusiana na
ushahidi uliotolewa kwa nia ya kujiridhisha kabla ya kutoa maamuzi
katika shauri hili.
UAMUZI
Kamati
imepitia vizuri mashtaka mawili dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na
ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji akiungwa mkono na ushahidi wa Ndugu
JAMES MHAGAMA ambaye alikuwa Mkoani Songwe wakati mashindano hayo
yakiendelea.
Pia Shahidi
ni mhanga wa vitendo visivyo vya kiungwana vilivyofanywa na Mlalamikiwa
dhidi yake ikiwepo kufikishwa mahakamani kwa madai ya fedha ambayo
yalilipwa na TFF lakini bado alifunguliwa kesi na kulazwa mahabusu baada
ya kukosa dhamana.
Hii yote ilitokana na udhaifu ulionyeshwa na Mlalamikiwa katika uaandaaji wa mashindano haya ya RCL Kituo cha Songwe.
Kamati
imeona kwamba TFF ilijitahi kuwa na mawasiliano yakaribu na Mlalamikiwa
ili kujitahidi kuepesha fedheha hiyo lakini hakuonyesha juhudi zozote
katika kutatua mgogoro huu zaidi ya kumtaka mimiliki wa hotel aendelee
kudai fedha yake kwakuwa wageni/Viongozi wa TFF wanakaribia kuondoka na
hata lipwa fedha zake jambo ambalo halikuwa na chembe ya ukweli.
Hivyo
Kamati imejiridhisha kwamba Mlalamikiwa alikuwa na nia mbaya dhidi ya
Shirikisho na hakujipanga kwa namna yoyote kuandaa mashindano haya na
kutoa taarifa zisizo sahihi kuwa Mkoa una uwezo wa kuandaa mashindano
jambo ambalo si kweli na kuonekana hana mahuasiano mazuri na viongozi
wenzake akiwemo Katibu wake ambaye alitoa ushirikiano mkubwa tangu
kuanza kwa mashindano hayo.
Pia
kitendo cha kutohudhuria kusikilizwa kwa shauri hili pasipo kutoa
udhuru wowote inaonekana jinsi Mlalamikiwa alivyokusudia kutotoa
ufafanuzi ambao ungekuwa ni utetezi wake kutokana na tuhuma ambazo
zinamkabili.
ADHABU
Baada
ya kupitia kwa kina ushahidi wa Mlalamikaji na vitendo vilivyoonyeshwa
na Mlalamikaj, Kamati inamtia hatiani Mlalamikiwa kwa kumpa adhabu ya
kutojihusisha na shughuli za Mpira wa miguu kwa kipindi cha miaka mitano
(5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka
2013.
Shauri la Pili
ATHUMAN KILUNDUMYA
Mlalamikiwa
hakuwepo katika kikao hiki isipokuwa aliwakilishwa na Ndugu MAULID
MWIKALO ambaye aliwasilisha mbele ya Kamati barua ya uwakilishi toka kwa
Mlalamikiwa.
Mwakilishi
alifafanua kwamba Mlamikiwa ni mtumishi wa Umma na ameshindwa kufika
mbele ya Kamati kwa kuwa ana majukumu mengine kwa Mwajiri wake Mkoani
Tabora.
Baada ya uthibitisho huo Kikao kiliazimia kuendelea na shauri kwakuwa Mwakilishi wa Mlalamikiwa alikuwepo.
Tuhuma
tatu ambazo zinamkabili Ndugu ATHUMANI KILUNDUMYA akiwa ni Katibu wa
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora kama ambavyo zinaonekana katika
hati ya mashtaka.
Mlalamikiwa
aliingiziwa fedha kiasi cha Tshs 680,000/= kwa ajili ya kuhudhuria
mkutano Mkuu wa TFF Jijini Arusha katika akaunti yake Namba 51001612542
iliyopo katika Benki ya NMB mnamo tarehe 29 Januari 2019 lakini
hakudhuria kikao hicho ingawa fedha alipata na hata alipotakiwa
kurejesha fedha hizo alikaidi maelekezo ya TFF.
Mlalamikiwa
pamoja na kutuma Mwakilishi aliwasilisha utetezi wake kwa njia ya
maandishi na katika tuhuma zote tatu alitoa majibu ya kufanana kuwa
hajawahi kupokea fedha hizo wala maelekezo ya namna ya kurejesha fedha
hizo na alijipanga kwa safari bahati mbaya safari yake iliishia Wilayani
Nzega baada ya kuitwa kazini na Mwajiri wake kwani yeye ni Mtumishi wa
Umma.
Hata hivyo
Mwakilishi wa Mlalamikiwa alifafanua kuwa ni kweli Mlalamikiwa
hakudhuria mkutano huo jijini Arusha pia ni hivi karibuni ndio amebaini
uwepo wa fedha katika akaunti yake kwa zaidi ya miezi mitano isipokuwa
mpaka sasa hajapewa utaratibu wa kurejesha, Iwapo atapewa utaratibu huo
yupo tayari kurejesha fedha hizo kiasi cha Tshs 680,000/=.
Kamati
ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi wa iwapo aliingiziwa fedha hizo
na kwakuwa hakuhudhuria Mkutano Mkuu Jijini Arusha kuanzia tarehe 2
Februari 2019 basi anapaswa kurejesha, Mwakilishi alikiri kuziona fedha
isipokuwa hajaambiwa taratibu za kurejesha na akipewa hata leo yupo
tayari kurejesha.
UAMUZI
Kamati
imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na
ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa maandishi wa
Mlalamikiwa ukiungwa mkono na ushahidi wa Ndugu MAULIDI MWIKALO, Kamati
imejiridhisha kwamba Mlalamikiwa ametenda makosa yote matatu na hakuna
utetezi wa msingi uliotolewa na ikizingatiwa kwamba maelezo yake na
ufafanuzi wa Mwakilishi unaonekana kukinzana. Fedha kiasi cha Tshs
680,000/= kiliingizwa kwa Mlalamikiwa kwa ajili ya kuhudhuria Mkutano
Mkuu wa TFF Jijini Arusha katika akaunti yake Namba 51001612542 iliyopo
katika Benki ya NMB mnamo tarehe 29 Januari 2019 lakini hakuhudhuria
kikao hicho ingawa fedha alipata na hata alipotakiwa kurejesha fedha
hizo alikaidi maelekezo ya TFF.
Mkanganyiko
wa maelezo yake unaonekana Mlalamikiwa si muaminifu pamoja kuwa ni
mtumishi wa umma na hakuwasilisha vielelezo vyote ili kuonyesha kwamba
alisafiri ingawa safari yake iliishia njiani na Mwakilishi wake hajui
aina ya usafiri ambao ulitumiwa na Mlalamikiwa wala tarehe ya safari
hivyo alikusudia kutumia fedha hizo kwa makusudi yasiyokusudiwa.
Mlalamikiwa
akiwa mtumishi wa Umma anafafahamu taratibu za kurejesha fedha ambazo
hazikutumika kwa lengo lililopangwa na kama angeona ni utaratibu tofauti
basi alipaswa kufanya mawasiliano na viongozi wake waliondaa Mkutano
huo jambo ambalo hakulifanya.
Maelezo kwamba fedha hii ameiona katika akaunti yake wiki moja iliyopita yanaonekana hayana ukweli wowote.
ADHABU
Baada
ya kupitia kwa kina ushahidi wa Mlalamikaji na vitendo vilivyoonyeshwa
na Mlalamikaji hasa ubadhirifu wa fedha za Taasisi, Kamati inamtia
hatiani Mlalamikiwa kwa kumtaka kwanza arejeshe fedha hizo kwenye
taasisi, pili kumpa adhabu ya kutojishusisha na shughuli za Mpira wa
miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya
Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka 2013 tatu,TFF kumchukulia Mlalamikaji
hatua za jinai iwapo itaona inafaa kwa ubadhirifu wa fedha alioufanya .
Shauri la Tatu
CONSTATINE MORANDI
Tuhuma
tatu ambazo zinamkabili Ndugu CONSTATINTE MORANDI akiwa ni Mwenyekiti
wa Geita Gold Football Club kama ambavyo zinaonekana katika hati ya
mashtaka.
Mlalamikiwa
alizuia kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV kwa mechi ya mchezo wa
mchujo play off kati ya timu yake dhidi ya Mwadui, Pia alikaidi maelekezo
ya ufafanuzi wa kuonyeshwa kwa mechi hiyo kutoka katika shirikisho na
kufanya vitendo vilivyoshusha hadhi ya TFF.
Mlalamikiwa
katika utetezi wake alikana tuhuma zote tatu kuwa hakuhusika katika
vitendo hivyo wala maandalizi ya mchezo huo kwa kuwa katika kipindi
chote hicho alikuwa wilayani Chato katika kikao cha Wenyeviti wa
Halmashauri kwa kuwa yeye ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji
Geita, hivyo alifika siku ya mchezo timu zikiwa tayari na maandalizi yote
yalifanywa na viongozi wenzake hasa Katibu wa Klabu ambaye ndiye
Mtendaji Mkuu wa shughuli za Klabu yao.
Aliiomba
Kamati imuone hana hatia kwakuwa hakuna mawasiliano yoyote aliyofanya
na TFF kwa niaba ya Klabu kuhusiana na mechi hiyo na hajawahi kuwazuia
watu wa Azam TV kuonyesha moja kwa moja (Mubashara) mechi yao ya mchujo
dhidi ya Mwadui, hivyo alimalizia kwa kusema hakushiri katika kikao
chochote cha maandalizi ya mechi hiyo kutokana kuwa nje ya Mji kwa muda
huo wakati maandalizi yanafanyika.
Kamati
ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi hasa ushiriki wake katika
kuzuia mechi, utendaji wa klabu yao namna mawasiliano yanavyofanyika ya
kutoka nje ya Klabu yao, Majibu yake ni kuwa Katibu wa Klabu ndiye
Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku na yeye huwa anapewa tu taarifa
na kubariki lakini hili la kuzuia mechi hakushirikishwa.
UAMUZI
Kamati
imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na
ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa Mlalamikiwa na kuona
kwamba upande wa Mlalamikaji umeshindwa kuthibitisha tuhuma zote tatu
dhidi ya Mlalamikiwa, Mlalamikiwa hakushiri kuzuia kuonyeshwa kwa mchezo
kwakuwa hakuna uthibitisho wowote uliotolewa, Hakuwahi kupewa maagizo au
maelezo yoyote toka TFF na kuyakaidi na wala hakufanya vitendo vyovyote
vile ambavyo vilishusha hadhi ya TFF Kinyume na Ibara ya 50 (1) vya
Katiba ya TFF. Hivyo kwa ujumla mashtaka dhidi yake hayajathibitishwa.
ADHABU
Baada
ya kupitia kwa kina tuhuma dhidi ya Mlalamikiwa, Ushahidi wa
Mlalamikaji na Utetezi wa Mlalamikiwa, Kamati imemuona Mlalamikiwa hana
hatia yoyote na inamuachia huru.
Shauri la Nne
SEIF KULUNGE
Tuhuma
tatu ambazo zinamkabili Ndugu SEIF KULUNGE akiwa ni Katibu wa Geita
Gold Football Club kama ambavyo zinaonekana katika hati ya mashtaka.
Mlalamikiwa
alizuia kuonyeshwa moja kwa moja na Azam TV kwa mechi ya mchezo wa
mchujo play off kati ya timu yake dhidi ya Mwadui. Pia alikaidi maelekezo
ya ufafanuzi wa kuonyeshwa kwa mechi hiyo kutoka katika shirikisho na
kufanya vitendo vilivyoshusha hadhi ya TFF.
Katika
shauri hili Mlalamikaji aliwasilisha vielelezo mbalimbali ambavyo ni
barua za mawasiliano kati ya Mlalamikaji, Bodi ya Ligi dhidi ya
Mlalamikiwa ili vielelezo katika ushahidi wake na Kamati ilivipokee kwa
kuwa hakukuwa na pingamizi lolote.
Shahidi
wa Mlalamikaji ambaye ni Msimamizi wa Matangazo ya Moja kwa moja kutoka
kituo cha Azam TV aliileza kamati kuwa alikuwa Geita katika Uwanja wa
Nyankumbu kwa ajili ya maandalizi ya kuonyesha mechi hiyo lakini
walizuiwa getini kwa maelezo kuwa mechi hiyo haitaonyeshwa mubashara la
sivyo watapasua gari la matangazo, Hivyo kama msimamizi alichukua jukumu
la kuwasiliana na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ambaye alimuunganisha
kwa kiongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoani Geita Ndugu PIUS KIMISHA
ambaye alimpa ushirikiano mkubwa, Kimsingi alieleza hakuwafahamu watu
hao isipokuwa lilikuwa ni kundi la Vijana waliokuwa getini kuanzia saa
tatu asubuhi hivyo mechi hiyo haikuonyeshwa kutokana na vitendo vya
vijana hao.
Mlalamikiwa
katika utetezi wake alikana tuhuma zote tatu kuwa hakuhusika katika
vitendo hivyo wala maandalizi ya mchezo huo kwa kuwa katika kipindi
chote hicho alikuwa anaumwa hapa Kigamboni Jijini Da Es Salaam na
hajaenda Geita zaidi ya Miezi sita.
Alifafanua
kuwa mnamo tarehe 2 Juni 2019 alipigiwa simu na Katibu wa TFF kwa
kumuuliza yupo wapi kwa wakati huo, ambapo baada ya muda kidogo alipigiwa
tena simu kuwa kuna watu wamezuia gari la matangazo la Azam TV na
alimjibu kuwa hafahamu watu waliozuia ingawa watu walikuwa wanahoji
uhalali wa matangazo hayo na faida kwa Klabu ukizingatia kuwa timu
inategemea viingilio vya mashabiki na Katibu akamsihi aruhusu na
matatizo hayo yatamalizwa. Shahidi anasema alifanya juhudi binafsi za
kuwasihi watangazaji wa Azam warejee kuonyesha mechi ambapo aliwasiliana
na Watangazaji hao ambao ni Pascal Kabombe na Ahmed pia alimtaarifu
Katibu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Miguu mkoa wa Geita lakini juhudi
zake hazikuzaa matunda. Azam TV walimjibu kuwa maandalizi yao yanachukua
muda mrefu hivyo hawako tayari kurejea na usalama wao ni mdogo hasa
mali.
Mlalamikiwa alikiri kuwa kulikuwa na mawasiliano baina yake na TFF pamoja na Bodi ya Ligi kwa emails na njia ya simu.
Kamati
ilimuuliza maswali ili kupata ufafanuzi hasa ushiriki wake katika
kuzuia mechi, utendaji wa klabu yao namna mawasiliano yanavyofanyika ya
kutoka nje ya Klabu yao, majibu yake ni kuwa hakuzuia mechi kuonyeshwa na
yeye kama Katibu wa Klabu ndiye Mtendaji Mkuu wa shughuli za kila siku
na yeye huwa anawasilisha taarifa za utendaji kwa Mkurugenzi wa Mji
kwakuwa timu hiyo si ya wanachama ni ya Halmashauri hivyo hakuna
viongozi wengine,Pia alikiri kuandika barua kwenda TFF ili kujua namna
ambavyo Klabu yao itanufaika na matangazo ya moja kwa moja ya mechi yao
na alipata ufafanuzi toka kwa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi.
UAMUZI
Kamati
imepitia vizuri mashtaka matatu dhidi ya Mlalamikiwa pamoja na
ufafanuzi uliotolewa na Mlalamikaji na utetezi wa Mlalamikiwa hasa
vielelezo na kubaini kwamba kulikuwa na mawasiliano ya pande tatu juu ya
uhalali wa mechi hiyo kuonyeshwa ambao ni Mlalamikaji, Bodi ya Ligi na
Mlalamikiwa jambo ambalo halikupingwa na Mlalamikiwa.
Kamati
imemtia hatiani Mlalamikiwa katika tuhuma zote tatu kwa kuwa ameonekana
kushiriki katika kuzuia, kukosa uaminifu ikizingatiwa alikiri kuwepo
mawasiliano baina yake na TFF na Bodi ya Ligi hasa barua yake ya
ufafanuzi kwenda Bodi ya tarehe 31 Mei 2019 yenye Kumb na. GGFC/350/GT
ambapo aliomba ufafanuzi wa mambo matano na ninakuu jambo la tano
aliloliomba "Natumaini mawazo na ombi letu kama hakuna majibu au malipo
ya pesa hatutakubali kuonyesha mubashara mechi yetu maana haina faida na
timu" Kauli hii inathibitisha namna ambavyo Mlalamikiwa alishiriki
katika kuhamasisha mechi isionyeshwe pamoja na kupewa ufafanuzi kutoka
Bodi ya Ligi, pia ni dhahiri kwamba hakuonyesha uaminifu kwa TFF
ikizingatiwa kwamba alifanya maawasiliano na kupewa ufafanuzi kuanzia
tarehe 31 Mei 2019 hadi 2 Juni 2019 na mwishoni akakiri makosa hayo kwa
kukiri makosa na kupokea ushauri kwa mikono miwili na kuahidi kuimarisha
ulinzi kwa mujibu wa email ya Mlalamikiwa kwenda TFF,vitendo hivyo
vilishusha hadhi kwa wadau mbalimbali waliohudhuria mechi hiyo tangu
siku ya kwanza.
ADHABU
Baada
ya kupitia kwa kina tuhuma dhidi ya Mlalamikiwa, Ushahidi wa
Mlalamikaji na Utetezi wa Mlalamikiwa, Kamati inamtia hatiani
Mlalamikiwa kwa kumpa adhabu ya kutojihusisha na shughuli za Mpira wa
miguu kwa kipindi cha miaka mitano (5) kwa mujibu wa Kanuni ya 73 ya
Kanuni za Maadili za TFF za Mwaka 2013.
Kwakuwa
vitendo vyake vingweza kuhatalisha usalama wa raia na mali zao hasa
wapenzi wa mpira waliofika uwanjani kwa siku hiyo,Kitendo hicho
kingeweza kuwaondoa Azam TV na wadhamini wengine kutodhamini mpira wa
miguu nchini Tanzania,Hivyo kama kuna hasara iliyotokea basi Mlalamikiwa
anapaswa kurejesha au kufidia hasara hiyo.
Wakili Kichere Mwita Waissaka
Mwenyekiti Kamati ya Maadili,TFF
Julai 5,2019
No comments:
Post a Comment