*Yatangaza neema kwa wachakataji mazao
kukuza uchumi wa viwanda
Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NMB PLC, imetoa wito kwa
Watanzania kutembelea Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Saba
Saba) ili kufungua akaunti za papo hapo kwenye banda lao.
Katika kuhakikisha benki hiyo
inaimarisha huduma zake za kifedha, imewahimiza watakaotembelea banda lao wawe
na vitambulisho ili wafungue akaunti za papo hapo na kuwa sehemu ya mabadiliko
ya kiuchumi nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana
kwa waandishi wa habari, Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Badru Idd alisema
wameamua kutoa huduma maalum na bora kwa wale watakaotembelea maonyesho hayo
yaliyoanza leo.
"Tutafungua akaunti ya chapchap, Akaunti
ya Mtoto, Akaunti ya Chipukizi na Akaunti ya Mwanachuo hapahapa Sabasaba,
ninatoa wito wa Watanzania kutumia jukwaa hili kufurahia benki nzuri na rahisi
na Benki ya NMB," alisema Badru.
Aidha, Benki hiyo imegeuza viwanja vya
Sabasaba kama tawi la benki kwa wateja wao ambapo huduma zote za kibenki zitatolewa,
wataweka, watatoa, huduma za ATM, NMB Wakala, ikiwa ni pamoja na huduma za
fedha za kigeni.
Badru alibainsha: "Huduma
zinazopatikana katika SabaSaba zinawahakikishia wateja kuwa si lazima kubeba
fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi ambao ni hatari kwa usalama; badala yake
wateja wanaweza kutoa fedha wakati wowote kutoka katika huduma zetu za ATM
zilizo na vifaa vizuri au NMB Wakala."
Katika hatua nyingine, Badru alisema
ili kuendana na kaulimbiu ya maonyesho hayo kwa mwaka huu ‘Usindikaji wa mazao
ya kilimo kwa maendeleo endelevu,’ NMB wameamua kutoa huduma maalumu kwa kuonyesha
bidhaa na huduma zinazotoa msaada mkubwa katika biashara ya kilimo ambayo ni
muhimu kufikia ajenda ya viwanda.
Kwa upande wake Meneja Mwandamizi Benki
ya NMB Idara ya Kilimo Biashara, Isaac Masusu alisema, benki hiyo imeanzisha utaratibu
wa kusaidia wataalamu wa kilimo kwa kutoa ufadhili wa kilimo nchi nzima.
"Tunao mtandao mkubwa wa matawi
ambayo huimarisha lengo la Kilimo, tumeunga mkono sekta ya kilimo kwa kutoa fedha
jumla ya Sh Bilioni 450 hadi sasa, pia tumewezesha mashirika zaidi ya 300 ya Wakulima
na bidhaa zitokanazo na mazao shambani, ikiwemo mashine kwa shughuli za viwanda
vya kuchakata mazao ya chakula,” alisema Masusu.
Wakati huo huo, NMB imewawezesha
wakulima zaidi ya 200,000 kupata huduma za kifedha,katika maeneo ambayo awali
hayakuwa na huduma hiyo hali iliyowasababisha watembee umbali mrefu.
No comments:
Post a Comment