HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 05, 2019

PINDA: WAFANYABIASHARA WENGI WAMEKUA KIBIASHARA

Na Tatu Mohamed

WAZIRI Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya mwaka huu hawezi kuyafananisha na maonesho mengine mengi yaliyopita.

Pinda ametoa kauli hiyo alipotembelea maonesho hayo ambayo ni ya 43 yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam.

"Nimetembelea mabanda mengi katika Maonesho haya ya 43, nimebaini mengi ikiwemo wafanyabiashara walioshiriki wamekua kibiashara, vifungashio vimeboreshwa, bidhaa  pamoja na kuwepo kwa mpangilio mzuri," amesema.

Hata hivyo, amesema kuwa pamoja na kuboreshwa maonesho hayo, Mamlaka husika zinazosimamia  na kudhibiti bidhaa na vyakula ikiwemo Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Shirika la Viwango Nchini (TBS) zisibweteke na badala yake ziendelee kusimamia zaidi ili waweze kushindana kimataifa.

"Biashara katika Maonesho haya   zimeboreshwa lakini pamoja na mafanikio haya Mamlaka zinazohusika na Udhibiti zisibweteke zikazane kusimamia zaidi ili tuweze kufika katika soko la ushindani la kimataifa"alisema Pinda

Ameongeza kuwa, kati ya vitu vingine alivyovibaini katika maonesho hayo ni kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa bidhaa za asali .

Pinda amesema katika Maonesho yaliopita bidhaa hiyo ilikuwa miongoni mwa bidhaa ambazo hazionekani zaidi.

"Nimefurahi pia kuona eneo la zao la asali limeonekana kuwa maarufu katika maonesho haya,nimekutana na watu wengi wanaouza zao hili.tuomba watu wajiwekeze zaidi katika zao hili kwa sababu soko lake ni zuri na linauwezekano mkubwa wa kukuza pato la na la taifa," amesema.

Aidha ametoa wito kwa Wananchi ambao hawajafika katika maonesho hayo kujitokeza kwa wingi kujionea mambo mbalimbali.

No comments:

Post a Comment

Pages