HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 02, 2019

TASAC YAONGEZEWA MAJUKUMU KATIKA KUONDOA SHEHENA BANDARINI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC), Emanuel Ndomba (kushoto), akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo. (Na Mpiga Picha Wetu).


Na Faraja Ezra, Dar es Salaam

SHIRIKA  la Wakala wa Meli Tanzania (TASAC) limeongezewa  majukumu ya  Uwakala wa Forodha  katika kusimamia uondoshaji wa shehena za bidhaa ikiwemo  Mbolea, Kemikali, Sukari viwandani, sukari za majumbani, Mafuta ya kupikia na Ngano.

TASAC pia ina jukumu la kusimamia masuala ya Madini, Makinikia,  Mitambo, Petroli, Wanyama hai pamoja na Nyara mbalimbali za serikali.

Akitolea ufafanuzi huo jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi  Mkuu wa Shirika Hilo, Emanuel Ndomba, alisema  Shirika limeongezewa majukumu ya kusimamia uondoshaji wa shehena bandarini pamoja na kudhibiti nyaraka za mizigo katika bandari.

Awali Ndomba akieleza majukumu ya Shirika kuwa ni kusimamia na kudhibiti shughuli za usafiri wa majinikwa ujumla wake Ila kwa Sasa limeongezewa majukumu.

Miongoni mwa majukumu hayo ni pamoja na kutoa leseni kwa watoa huduma kwa kuzingatia  sheria na kanuni  ili kulinda usalama wa abiria na mizigo yao.

Aidha TASAC pia ina majukumu ya kusimamia uhakiki wa Mizigo mbalimbali inayoingia na kutoka  bandarini.

Mkurugenzi huyo alisema  majukumu hayo yameongezwa na serikali baada ya Bunge la bajeti  la 2019 kupitisha azimio hilo na kuweka utaratibu  wa utekelezaji  na migawanyo ya kazi katika Shirika hilo.

"Mikakati iliyopo  sasa ni kuhakikisha  shirika linatoa huduma bora kwa wateja kwa  kuzingatia sheria na kanuni zlizowekwa na mamlaka husika," alisema Ndomba.

Ndomba alisema shirika limejipanga  vema kukabiliana na majukumu yaliyoongezwa na kuweka mikakati ya kiutendaji kuhakikisha unafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Hata hivyo shirika limepata pia fursa ya kusimamia Meli zinazosafirisha  vimiminika ikiwemo gesi, mafuta na bidhaa ikiwemo Meli ya kitalii, Meli ya magari, Meli za maonyesho Meli za kukodi na Meli za kijeshi.

No comments:

Post a Comment

Pages