HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

July 07, 2019

TRC kufunga njia za reli kwa saa 72 ili kukarabati reli ya kati

Na Janeth Jovin

SHIRIKA la Reli Tanzania (TRC) limebadilisha ratiba zake za usafirishaji wa treni za bara na Mjini ili kuwezesha ukarabati unaoendelea kumalizika kwa wakati.

Aidha Shirika hilo limewahakikishia wakazi wa Mikoa ya Kaskazini kuwa ifikapo Desemba itatolewa treni maalum kwaajili ya wanaokwenda kusherehekea sikukuu ya Krismas.

Akizungumza na waandishi wa habari jana katika banda lao lililopo kwenye maonesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) maarufu sabasaba, Mkurugenzi wa TRC, Masanja Kadogosa (pichani), anasema shirika hilo lipo katika utekelezaji wa mradi wa uboreshaji wa reli ya kati Dar-Isaka ambao ulianza rasmi Juni, 2018 na unatarajia kukamilika mwaka 2020.

Anasema ili kuwezesha ukarabati huo kukamilika kwa wakati, TRC litalazimika kufunga njia kwa masaa 72 kila wiki kwa muda wa miezi mitano.

Anasema katika kipindi hicho watapoteza zaidi ya Sh. Bilioni 1.8 za mapato ya ndani.

“Huwezi kuwa na Tanzania ya Viwanda bila kuwa na uhakika wa usafirishaji wa bidhaa zako. Shirika letu linapitia katika matengenezo, au ukarabati wa njia ya km 970 kutoka Dar es Salaam hadi Isaka, kwahiyo shughuli lazima zitapungua.

“Tulipoanza mwanzo tulikuwa kwa siku tunafunga kwa masaa 6 mpaka 8, lakini kwa hatua iliyofikiwa sasa tumeamua kufunga kwa masaa 72. Hivyo kuanzia leo tarehe 7 hadi 13 tunaanza rasmi, kwahiyo treni za bara zitapungua mpaka tatu na treni za Mjini zitapungua kutoka 6 mpaka 5,” anasema.

Alitaja kuwa treni za Mjini zitakuwepo siku ya Jumatatu mpaka Ijumaa, safari za kutoka Dar es Salaam, Mwanza na Mpanda itakuwepo kila Jumatatu na Jumatano huku safari ya kutoka  Mwanza na Kigoma kuja Dar es Salaam itakuwepo siku za Jumatano na Jumapili.

Aliongeza kuwa, kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma itakuwepo kila Jumanne na kutoka Kigoma kuja Dar es Salaam treni itakuwepo kila Alhamisi.

“Lakini kitu ambacho naweza kuwahakikishia wakazi wa Kaskazini kuwa Krismas inayokuja wataenda na treni yao, shirika la reli litatoa treni special, badala ya kuendesha magari watatumia treni, na tutafanya utaratibu pia iwarudishe.

“Kwahiyo mwezi wa 12 tunawahakikishia wakazi wa kaskazini watakuwa na treni ya abiria ya kwenda huko kwa mara ya kwanza,” anasema.

Aidha Kadogosa, anasema ndani ya wiki mbili zijazo TRC itafungua njia kutoka Tanga hadi Moshi, ambapo wataanza majaribio kwa treni ya mzigo.

No comments:

Post a Comment

Pages