Na Tatu Mohamed, Dar es Salaam
MAMLAKA
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Songea imebuni mashine ndogo ya
kubangulia korosho ambayo ina uwezo wa kubangua debe tatu kwa siku,
huku ikiwa na uwezo wa kutenganisha ubora wa bidhaa hiyo.
Mwalimu
kutoka VETA Songea, Susack Mbulu, amesema hayo katika banda la VETA,
lililopo katika maonesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa (DITF),
yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa,
jijini Dar es Salaam.
"Ukitumia
mashine hii, unaweza kutenganisha korosho kwa ubora, yaani kama ni
daraja la kwanza hadi la tatu. Na iwapo mtumiaji wa mashine hii
ataanza kubangua bila kukausha korosho hizo vyema zitavunjika na
iwapo zitakauka hazitovunjika bali zitatoka sawa," amesema.
Ameongeza
kuwa mashine hiyo inauwezo wa kuanza kubangua korosho ndogondogo ama
zilizo kubwa kwa kuwa ina meno ya aina mbili ambayo kwa pamoja yanaweza
uwezo wa kubangua zao hilo na kumrahisishia mkulima mdogo.
Amesema mashine
hiyo inatumia nguvu za binadamu na itawasaidia wazalishaji wadogo
kuondokana na mfumo wa kukoka moto na kukaanga korosho na kisha
kuanza kuzipasua kwa mkono, badala yake sasa watatumia mashine
hiyo.
Hata
hivyo, Mbulu ameushukuru uongozi wa VETA makao makuu kwa
ushirikiano wao na kuwezesha kutekeleza wazo hilo, ambalo
linaunga mkono dhana ya serikali ya kufikia uchumi wa kati
ambao ni wa viwanda.
Amesema
katika kufikia uchumi wa viwanda VETA inaunga mkono jitihada hizo
ambapo wataweza kuwafikia na kuwasaidia wajasiriamali wadogo.
Lakini pia kusaidia korosho kuingia sokoni katika hali ya
ubora.
"Lengo letu ni
kuhakikisha mashine hii inafikia kiwango cha kutumia umeme au mota
ambayo itafikisha hatua ya kubangua hata gunia moja kwa siku la
korosho," amesema.
Aidha
amewashauri wafanyabiashara wa korosho kuwasiliana na VETA ili
kuweza kupata mashine hiyo na kuahidi kuwa wanaweza kuifikisha
serikali katika uchumi wa viwanda.
No comments:
Post a Comment