Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizunguma na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa
wakati alipokwenda ofisi za Shirika hilo kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya
pango la ardhi jijini Dar es Salaam. Wengine pichani ni maofisa kutoka Wizara
ya Ardhi pamoja na Shirika la Reli.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa wakati wa kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosa wakati wa kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoka
katika ofisi za Shirika la Masoko Kariakoo wakati alipokwenda ofisi za Shirika
hilo kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akizungumza na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Taifa cha Utalii Boniface Mwaipaja wakati
alipokwenda ofisi za Chuo hicho kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya pango la
ardhi jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akipokewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania Masanja Kadogosi
mara baada ya kuwasili ofisi za Shirika hilo kufuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya
pango la ardhi jijini Dar es Salaam. (Picha na Wizara ya Ardhi).
Na Munir
Shemweta
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk. Angeline Mabula, ameanza operesheni maalum ya
kuzibana Taasisi ambazo ni wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi katika jiji
la Dara es Salaam kwa kutembelea ofisi moja hadi nyingine ili zilipe madeni yao
katika muda uliopangwa ambapo katika ziara hiyo taasisi sita kati ya saba alizotembelea
zimeahidi kulipa zaidi ya bilioni 4.5 kufikia Desemba 2019.
Dkt Mabula alizitembelea
taasisi hizo juzi ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi kuhakikisha wadaiwa wote sugu wa kodi ya pango la ardhi wanalipa madeni
yao kabla ya hatua za kuwafikisha kwenye Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya wale
watakaokaidi kulipa ambapo adhabu yake ni kulipa ama kupigwa mnada kwa mali za
taasisi husika kufidia deni la kodi ya pango la ardhi.
Taasisi alizotembelea
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi juzi ni Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO) linalodaiwa bilioni 3, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) bilioni 1.4,
EPZA milioni 200, Shirika la Reli Tanzania (TRC) bilioni 2.5, Shirika la Masoko
Kariakoo milioni 249 pamoja na Chuo cha Taifa cha Utalii milioni 26.8.
Akiwa katika Shirika la
Masoko Kariakoo, Dkt Mabula alishangazwa na Shirika hilo kudaiwa zaidi ya
milioni mia mbili huku likiomba kulipa deni lake katika kipindi cha miaka
miwili jambo alilolieleza kuwa ni kinyume na taratibu za ulipajia madeni ya
kodi ya pango la ardhi ambazo humtaka mdaiwa kulipa nusu ya deni.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu
wa Shirika la Masoko Kariakoo Bw. Hetson Kipsi katika barua yake, Shirika lake
liliahidi kulipa kwa awamu deni hilo katika kipindi cha miaka miwili kwa kutoa
milioni saba kila mwezi jambo lililokataliwa na Dkt Mabula ambapo alieleza kuwa
Shirika hilo linapaswa kulipa nusu ya deni kwanza ndipo liingia makubaliano ya
kulipa kiasi kilichobaki kwa awamu. Hata hivyo Shirika la Masoko Kariakoo lilikubali
kutoa milioni mia moja kufikia 29 Julai 2019 na kukamilisha kiasi kilichobaki desemba
2019.
Kwa upande wa Shirika
la Reli Tanzania (TRC) Mkurugenzi Mtendaji wake Masanja Kadogosa alimueleza
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Mkazi Dkt Mabula kuwa Shirika lake
halipingi kulipa deni inalodaiwa bali inachofanya ni kuhakiki upya deni hilo
kwa kuwa kumekuwa na uhamisho wa umiliki wa mali za TRC kwenda TBA tangu mwaka
1999 sambamba na baadhi ya nyumba za Shirika kuuzwa kwa wananchi huku baadhi ya
mali za TRC zikiwa hazina hati.
Kadogosa alisema, kiasi
cha shilingi bilioni 2.4 wanachodaiwa ni kikubwa na hakilingani na uhalisia wa
deni la TRC na kubainisha kuwa uhakiki utakapokamilika ana imani deni hilo litapungua
kwa kiasi kikubwa. Dkt Mabula alimueleza kuwa, Shirika lake linapaswa kulipa
robo ya tatu ya deni hilo wakati uhakiki ukiendelea na iwapo itaonekana deni limepungua
basi kiasi cha fedha kilichozidi kitarudishwa. Hata hivyo, Mkurugenzi huyo Mtendaji wa TRC alikubali
kulipa kiasi cha milioni 400 kwa awamu hadi kufikia oktoba 2019 wakati zoezi la
uhakiki wa deni hilo unaohusisha Wataalamu wa Shirika hilo na Wizara
ukiendelea.
Chuo cha Taifa cha
Utalii kupitia kwa Kaimu Mkuu wa Chuo Boniface Mwaipaja kilikiri kudaiwa kiasi
cha milioni 26.8 na kuahidi kulipa kwa awamu deni hilo ambapo Mkuu huyo wa Chuo
aliahidi kulipa kiasi cha milioni saba kwanza na baadaye kulipa kwa awamu kiasi
kilichobaki na kukamilisha deni hilo kufikia desemba 2019.
Taasisi nyingine
zilizotembelewa na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na
kuahidi kulipa madeni yao baada ya uhakiki ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) inayodaiwa
bilioni 1.4, na EPZA milioni 200 ambapo kwa upande wake TBA tayari imeandaa
utaratibu wa kulipa deni hilo kwa awamu na tayari milioni 40 zimetengwa wakati
EPZA ilihidi kutoa mchanganuo wa jinsi itakavyolipa deni hilo wiki hii.
Juni 11, 2019 Wizara ya
Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi iliitisha kikao cha Taasisi ambazo ni wadaiwa
Sugu wa kodi ya Pango la Ardhi takriban 200 kwa kuwapa taarifa ya kulipa madeni
yao sambamba na kuhakiki madeni hayo kabla ya hatua za kisheria hazijachukuliwa
kwa watakaokaidi kulipa madeni hayo. Ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ilikuwa ni kuangalia taasisi
zinazodaiwa zimekwama wapi kutekeleza agizo lililotolewa.
No comments:
Post a Comment