*Awaonya vijana,
wazee wanaotaka kuwaoa, asema miaka 30 jela ni yao
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watoto wa kike
wasikubali kudanganywa na wanaume na badala yake wakazanie masomo hadi wahitimu
elimu ya juu.
“Wasichana wote mliopo hapa, mwanaume yeyote akikufuatafuata mwambie
usinusumbue; mwambie niache nisome. Kamwe msikubali kudanganyika, someni
hadi mmalize Chuo Kikuu,” alisema.
Ametoa wito huo kwa nyakati tofauti wakati
akizungumza na wakazi wa wilaya za Same na Mwanga akiwa kwenye ziara ya kikazi
ya kukagua shughuli za maendeleo mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa na ziara ya siku nne
mkoani humo, amewaonya vijana na wazee ambao wana tabia ya kuweka mahusiano ya
kimapenzi na watoto wa kike kwamba waache mara moja la sivyo wataishia
jela.
“Wanaume msisahau kwamba mtoto wa mwenzio ni wako.
Nataka niwakumbushe kuwa ukimuona mtoto wa kike, muache. Huyo ni moto wa kuotea
mbali. Ukimchumbia, ukimuoa, au kumpa mimba mtoto wa kike, ujue kuwa miaka 30
jela ni yako.”
“Serikali ya awamu ya tano, imeamua kuwekeza kwa
mtoto wa kike, kwa hiyo tunataka watoto wa kike wakianza shule ya awali, wasome
shule ya msingi, waende sekondari hadi wamalize Chuo Kikuu,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment