WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi
wa Elimu ya Juu (HESLB),
kutafakari namna ya kurekebisha baadhi ya dosari zilizopo likiwemo suala la kuwanyima mikopo wanafunzi kwa kutumia kigezo cha kusoma katika shule binafsi.
kutafakari namna ya kurekebisha baadhi ya dosari zilizopo likiwemo suala la kuwanyima mikopo wanafunzi kwa kutumia kigezo cha kusoma katika shule binafsi.
Amesema
kuna baadhi ya wanafunzi ambao wamefaulu vizuri kidato cha nne na
wamekosa nafasi katika shule za Serikali na wanatoka katika familia
zisizokuwa na uwezo, hivyo wanatafuta wafadhili ambao wanawasomesha
kwenye shule binafsi.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumamosi, Agosti 10, 2019) wakati akifungua
mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jumuiya ya Wanafunzi wa Taasisi za Elimu ya
Juu Tanzania (TAHLISO) kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM).
Amesema
kitendo cha bodi hiyo kuwanyima mikopo baadhi ya wanafunzi kwa kigezo
cha kusoma katika shule binafsi bila ya kujiridhisha kama wanatoka
kwenye familia zenye uwezo au zisizokuwa na uwezo kinawanyima wanafunzi
hao fursa za kuendelea na masomo.
Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaonya wakuu wa vyuo vikuu ambao wanatumia
vibaya fedha za mikopo ya wanafunzi kwa kuzipeleka katika miradi
mbalimbali baada ya kuzipokea kutoka HESLB na kuwacheleweshea wanafunzi
stahiki yao.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa vyuo vikuu kuimarisha mafunzo kwa
njia ya vitendo kwani tafiti nyingi zinazohusu mambo ya ajira
zimebainisha umuhimu wa mafunzo ya vitendo katika kumuwezesha mhitimu
kuwa na uelewa na ujuzi mpana wa kile alichokisoma kwa njia ya nadharia.
“Vyuo
viongeze umakini na ufuatiliaji wa karibu wa vijana wetu wanapokuwa
kwenye elimu kwa vitendo ili kuhakikisha kwamba wanapata maarifa na
ujuzi uliokusudiwa katika mitaala yao. Pia natoa wito kwa waajiri wa
sekta ya umma na binafsi watoe ushirikiano wa dhati kwa wanafunzi
wanaotafuta nafasi za kufanya mafunzo kwa njia ya vitendo kwenye taasisi
zao.”
Kwa upande wake,
Mwenyekiti wa TAHLISO, Bw. Peter Niboye amesema miongoni mwa changamoto
zinazowakabili wanafunzi wa elimu ya juu ni ucheleweshwaji wa mikopo
kwa baadhi ya vyuo licha ya HESLB kuwasilisha fedha hizo mapema, hivyo
ameiomba Serikali kuwasaidia katika kutatua tatizo hilo.
Kadhalika,
Mwenyekiti huyo wa TAHLISO, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa ushirikiano mkubwa
inaoipatia jumuiya hiyo hivyo kurahisisha utendaji wake.
Awali,
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Bw. Patrobas Katambi alimkabidhi Waziri Mkuu
hati ya kiwanja kilichoko katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kwa ajili
ya ujenzi wa ofisi za TAHLISO, ambapo baada ya kupokea hati hiyo, Waziri
Mkuu aliikabidhi kwa Mkwenyekiti wa jumuiya hiyo Bw. Niboye.
Mkutano
huo umehudhuriwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce
Ndalichako, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Paul Makonda, Mkuu wa
Wilaya ya Kinondoni, Bw. Godfrey Chongolo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Bw.
Kisare Makori pamoja na viongozi kutoka vyuo mbalimbali nchini
vinavyounda TAHLISO.
No comments:
Post a Comment