Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akionyesha kitabu cha Bima ya Mazao wakati wa uzinduzi wa Bima ya Mazao uliofanyika kwenye Banda la NHC wakati wa maonesho ya wakulima (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, jana tarehe 4 Julai 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akimkabidhi katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe bidhaa na muongozo wa Bima ya Mazao wakati wa uzinduzi wa Bima ya Mazao uliofanyika kwenye Banda la NHC wakati wa maonesho ya wakulima (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, jana tarehe 4 Julai 2019. Mwingine Pichani (Katikati) ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe Antony Mtaka.
Waziri wa Kilimo Mhe. Japhet Hasunga (katikati), Mkurugenzi Mkuu wa NIC Dkt. Elirehema Doriye, akifuatiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Ushirika Dkt.Titus Kamani, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. Antony Mtaka pamoja na viongozi wengine wa sekta ya kilimo na Ushirika wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Vyama vya ushirika waliopata vyeti vya utambuzi kwa mchango katika Kilimo na Ushirika, jana tarehe 4 Julai 2019.
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akihutubia wananchi waliojitokeza wakati wa uzinduzi wa Bima ya Mazao kwenye Banda la NHC wakati wa maonesho ya wakulima (Nanenane) kwenye viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu, jana tarehe 4 Julai 2019.
Na Mathias Canal,
Wizara ya Kilimo-Simiyu
Katika miaka ya karibuni,
Wizara ya Kilimo imebuni mbinu
mbalimbali za kubadili wakulima kutoka katika kilimo cha kujikimu na kuwa
cha biashara. Kwa upande mwingine, kilimo ni
biashara yenye vihatarishi vingi kwa wakulima wa Tanzania na Bara la Afrika,
Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa ujumla.
Hali hii
imesababishwa na kutegemea mvua, mabadiliko ya hali ya hewa, moto, uharibifu wa
ndege na wanyama, magonjwa ya mimea, upepo mkali, mbegu na dawa za wadudu nk.
Mara nyingi, hakuna uwiano kati ya
wakulima wadogo na wakubwa katika sekta ya kilimo katika matumizi ya
teknolojia, ufikiaji wa soko, kusimamia
hatari zisizodhibitiwa, utoaji wa elimu na uhamasishaji, mikopo na huduma za
bima.
Waziri wa Kilimo
Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameyasema hayo jana tarehe 4 Julai 2019 wakati
akizundua Bima ya Mazao ambapo alisisitiza kuwa, kuanzisha Bima ya Mazao ni muhimu kwa wakulima nchini
Tanzania ili kukabiliana na hasara zitokanazo na vihatarishi vinavyoathiri
uzalishaji.
Mhe Hasunga
alisema kuwa kuna kampuni kadhaa za Bima
ambazo zimeanzisha bidhaa mbalimbali za bima kwa ajili ya kumkinga mkulima dhidi
ya hasara kwa aina tofauti za mazao. Kampuni hizo ni pamoja na Kampuni ya Bima
ya Taifa (NIC), Jubilee na UAP.
Hata hivyo, utoaji
wa bidhaa za bima ya mazao umekuwa ukifanyika bila mwongozo thabiti ambao ungewanufaisha
wakulimna wengi wadogo hususan maeneo ya vijijini. Hivyo, mwongozo huu
unaolenga kubainisha namna bima ya mazao inavyoweza kuwakinga wakulima dhidi ya
hasara una umuhimu wa kipekee kwa wakati huu wa mapinduzi makubwa ya sekta ya kilimo nchini.
Alisema kuwa Bima ya mazao aliyoandaliwa na NIC kwa
kushirikiana na Wizara ya kilimo iliyozinduliwa ni faraja kubwa kwa wakulima
nchini.
Uandaaji wa Bima
ya mazao iliyozinduliwa pamoja na Mwongozo vimezingatia: Dira ya Maendeleo ya Taifa
(Tanzania Development Vision 2025); Mpango wa Taswira ya Muda Mrefu wa
Taifa (Long Term Perspective Plan -LTPP 2012-2021); Mpango wa Pili wa
Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (Five Year Development Plan II - FYDP II
2016-21); Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (Agricultural
Sector Development Program II – ASDP II ). Vilevile, Sheria ya Bima Namba 10
ya mwaka 2009 (Tanzania Insurance Regulatory Authority Act. No. 10 of 2009)
imezingatiwa.
Mhe Hasunga
amesema kuwa Miongoni mwa manufaa yapatikanayo kutokana na kuwepo kwa mwongozo
wa Bima ya Mazao ni pamoja na kutoa fursa kwa wakulima kupata aina sahihi ya bidhaa
ya bima ya mazao kutoka kwa kampuni za bima zenye vibali na zilizosajiliwa, kuwapa
wakulima uwezo wa kuchagua aina ya bima ya mazao waipendayo, na kuwezesha
wakulima kubadili tabia ili kufuata kanunu bora za kilimo.
Zingine ni kudhibiti
kampuni zinazotoa huduma za bima ya mazao ili kubuni bidhaa za bima ya mazao
ambazo zina manufaa makubwa kwa wakulima, kujenga uaminifu miongoni na taasisi
za fedha kwa kutoa mikopo ya kilimo na kuweka mazingira wezeshi kwa wakulima katika
taratibu za kujiandikisha, kuwasilisha madai, kinga ya mazao na taratibu za
malipo pindi hasara inavyotolewa taarifa.
Kadhalika Mhe
Hasunga alisema kuwa utekelezaji wa Mwongozo huo kwa ukamilifu, utawezekana ikiwa
kutakuwa na juhudi za pamoja kati ya Wizara ya Kilimo na wadau wengine
wanaojishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na biashara.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na
Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, imeendelea
kuimarisha na kuendeleza ukuaji wa Sekta ya Kilimo Nchini kutumia programu mbali mbali kwa kushirikiana na wabia wa
maendeleo ya kilimo.
Uendelezaji wa sekta hii ya kilimo ni muhimu katika
kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa, unaopelekea ukuaji wa sekta ya viwanda, upatikanaji
wa chakula na lishe ya kutosha kwa Watanzania na uzalishaji wa kibiashara. Kwa
sasa, sekta ya kilimo inachangia 29.1% ya Pato la Taifa, 65.5% ya ajira, 65% ya malighafi za sekta ya viwanda na 30%
ya mapato yatokanayo na mauzo ya nje ya
nchi.
No comments:
Post a Comment