HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

August 04, 2019

Rais Magufuli kufungua Wiki ya Viwanda SADC

Na Suleiman Msuya

RAIS John Magufuli leo anatarajiwa kufungua maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda ya Jumuiya ya Maendeleo Kisini mwa Afrika (SADC), yanafanyika jijini Dar es Salaam.

Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda yanaanza leo hadi Agosti 9 mwaka huu ikiwa ni maandalizi ya kuelekea mkutano wa 39 wa wakuu wa nchi 16 za SADC unatarajiwa kufanyika kuanzia Agosti 17 na 19/2019.

Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhandisi Stella Manyanya alisema maonesho hayo yamepata bahati ya kufunguliwa na Rais Magufuli hivyo kuwataka wafanyabiashara na wazalishaji wasimuangushe.

Alisema hadi sasa zaidi ya wafanyabiashara na wazalishaji 2,000 wamejisajili kushiriki Wiki ya Viwanda ambapo zaidi ya 1,700 ni wazawa.

Naibu Waziri Manyanya alisema katika ya washiriki hao 2,000 washiriki 938 ni watakaofanya maonesho huku wengine wakishiriki kongamano.

"Wiki ya Viwanda imepata bahati ya kufunguliwa na Rais Magufuli na kufungwa na Rais wa Zanzibar, Dk.Ali Muhammed Shein ni imani yangu washiriki watatumia nafasi hiyo kuthibitisha ubora wa wanavyozalisha," alisema.

Mhandisi Manyanya aliwataka Watanzania hasa wafanyabiashara na wazalishaji kutumia wiki hiyo kujenga ushirikiano na wenzao wa nchi wanachama wa SADC.

Alisema mkutano huo ni fursa ya kipekee ambayo Tanzania imeipata hivyo ni imani yake itatumika vizuri na kwamba Serikali kupitia wizara ya Viwanda na Biashara ipo tayari kusaidia.

Naibu Waziri Manyanya alisema Tanzania ina rasilimali nyingi zinazohitajika ukanda wa SADC hivyo zinapaswa kutangazwa ili ziweze kuwa na tija kwa nchi na wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Viwanda na Ushindani Sekretarieti ya SADC, Johansein Rutaihwa alisema Wiki ya Viwanda ya SADC ni fursa muhimu kiuchumi hivyo kuwataka washiriki kuitumia kwa umakini.

Rutaihwa alisema nchi wanachama wa SADC zina wananchi zaidi ya milioni 300 hivyo ni soko la uhakiki kwa Tanzania na nchi zingine kulitumia.

"SADC mwaka 2015 ilikuja na mkakati unafikia kikomo mwaka 2063 ambao unataka kuwepo mapinduzi ya sekta ya viwanda kwa nchi wanachama hivyo kupitia wiki hii ndio fursa zinapoonekana naomba tuzitumie," alisema.

Alisema Mkakati wa Viwanda nchi wanachama (SISR) unaotaka nchi wanachama kuingia katika mfumo wa viands vinavyotumia teknolojia na kuachana na rasilimali ifikapo 2063 umeonesha matokeo chanya.

Mkuu huyo wa Kitengo alisema hadi sasa nchi zote zimeonesha dhamira ya kutekeleza mkakati huo wa SISR ambapo nchi tisa zimeanza utekelezaji wa kivitendo.

No comments:

Post a Comment

Pages