NA SULEIMAN MSUYA
JUMUIYA
ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), imesema inaendelea na
mchakato wa kuunda Mfuko wa Kilimo wa Kanda kwa ajili ya kusaidia nchi
wanachama katika sekta ya kilimo.
Hayo
yamesemwa na Mkurugenzi wa Chakula, Kilimo na Maliasili (FANR) SADC,
Domingo's Gove wakati akielezea majukumu ya idara yake kwa waandishi wa
habari jana jijiji Dar es Salaam.
Alisema
sekta ya kilimo ni muhimu katika kuchochea maendeleo na uchumi wa nchi
16 za SADC hivyo ni wakati muafaka wa kuja na mfuko huo.
Alisema
sekta ya kilimo inakabiliwa na changamoto mbalimbali kama mabadiliko ya
tabia nchi, wadudu vamizi kama viwavijeshi ambapo njia ya kukabiliana
navyo ni kuwepo na chombo rasmi kwa ajili hiyo.
"Katika
kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija kwa nchi wanachama tupo
kwenye mchakato wa kuja na mfuko wa kilimo ambao utasaidia nchi zote,"
alisema.
Alisema mfuko huo utasaidia upatikanaji wa mbegu bora, mbolea, dawa na kusaidia kilimo cha umwagiliaji kwa wakulima.
Gove alisema iwapo kila nchi itashiriki kikamilifu ni dhahiri sekta hiyo itachangia uchumi na maendeleo kwa kasi.
"Zipo mbegu zaidi ya 48 katika nchi wanachama za SADC ambazo wanazipa kipaumbele kulingana jiografia ya nchi husika," alisema.
Alisema mkakati wao ni kuwa na mbegu amabazo hazishambuliwi na wadudu vamizi kama viwavijeshi.
Mkurugenzi huyo alisema mfumo huo utasaidia utekelezaji wa vipaumbele vinne vya SADC katika sekta hiyo muhimu.
Alitaja vipaumbele vinavyosimamiwa na idara yake ni pamoja kukuza uzalishaji na ushindani katika sekta.
Pia
alisema idara hiyo imejipanga kutafuta na kutangaza masoko, kuhamasisha
sekta binafsi katika uwekezaji na kuongeza usalama wa chakula.
Aidha,
mkurugenzi huyo alisema mipango na mikakati ambayo inatekelezwa na SADC
itakuwa na tija iwapo itashabiahiana na Sera za nchi wanachama katika
sekta husika.
Alisema
sekta ya kilimo inaweza kuleta mapinduzi iwapo itashabihiana na uwepo wa
viwanda, miundombinu, ulinzi na usalama na program maalum ambapo
Tanzania imeonesha mfano.
Kwa
upande mwingine Gove amezikumbusha nchi za SADC kutekeleza azimio
walilokubaliana viongozi kwa kutenga asilimia 10 katika Bajeti za nchi
kuelekezwa Bajeti ya kilimo.
Alisema sekta hiyo ikipewa kipaumbele nchi na wananchi watafanikiwa kiuchumi na maendeleo
No comments:
Post a Comment